Sunday, 11 October 2026

MAHAKAMA WILAYA YA RUANGWA YAWAHUKUMU WATANO KWA UKITILI WA MTOTO

Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi imewahukumu watu watano, wakiwemo mama mzazi wa mtoto, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ukatili kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mhe. Jonas Lyakundi alisema washtakiwa hao walihusika katika tukio lililotokea Aprili 08, 2026 majira ya saa 1 jioni […]

Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi imewahukumu watu watano, wakiwemo mama mzazi wa mtoto, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ukatili kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mhe. Jonas Lyakundi alisema washtakiwa hao walihusika katika tukio lililotokea Aprili 08, 2026 majira ya saa 1 jioni katika Kijiji cha Gogovivu, Wilaya ya Ruangwa, ambapo walimfanyia ukatili mtoto huyo kwa kumchoma kwa kutumia jalo (bati) lililokuwa na moto, wakimtuhumu kwa madai ya kuiba fedha za mama yake mzazi.

Washtakiwa hao ni Rehema Athuman Mnonda (31) ambaye ni mama mzazi wa mtoto, Maduna Abdallah Kumbugo (51) bibi mzaa mama wa mtoto, Khadija Athuman Mnonda (32), Awesa Issa Luangai (21) pamoja na Nurathi Mbaraka Linyatu (16).

Inadaiwa kuwa baada ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi, washtakiwa wote walikamatwa na kufikishwa mahakamani Mei 21, 2026 ambapo walikiri kosa, kabla ya hukumu kutolewa Juni 03, 2026.

Katika hukumu hiyo, washtakiwa namba 1 hadi 4 wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani pamoja na kulipa fidia ya shilingi 100,000 kila mmoja kwa mhanga, huku mshtakiwa namba 5, Nurathi Mbaraka Linyatu (16), akipewa adhabu ya kufanya kazi za jamii mara mbili kwa wiki kwa kipindi cha miaka miwili.

Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Diana Lukondo akisaidiwa na John Remmy aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa jamii dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *