Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Nurdin Babu, imetembelea na kukagua miradi mbalimbali itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi yake mkoani humo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamati hiyo imewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru utakapowasili katika maeneo yao, huku ikieleza kuwa miradi hiyo inalenga kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha mafuta Sango kilichogharimu shilingi milioni 250, mradi wa Box Culvert Ushiri Ikuini wenye thamani ya zaidi ya milioni 43, pamoja na ujenzi wa jengo la maktaba na TEHAMA katika Shule ya Sekondari Mashati uliogharimu zaidi ya milioni 154.
Miradi mingine ni ujenzi wa ofisi ya kijiji Ngaseni uliogharimu zaidi ya milioni 31, mradi wa utengenezaji wa matenga ya nyanya wa kikundi cha Umoja wa Vijana Tarakea Motamburu wenye thamani ya zaidi ya milioni 12, ujenzi wa Zahanati ya Ubaa uliogharimu zaidi ya milioni 350, pamoja na uboreshaji wa mradi wa maji Lake wenye gharama ya zaidi ya bilioni 1.8.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa mkoani Kilimanjaro tarehe 28 Juni 2026 katika Tarafa ya Hedaru ukitokea Mkoa wa Tanga Region, kabla ya kuwasili Wilaya ya Rombo District tarehe 30 Juni 2026.
Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 inasema: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”
