Israel na Lebanon zimekubaliana kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, imeeleza kuwa makubaliano hayo yanatokana na kusitishwa kabisa kwa mashambulizi yanayofanywa na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran pamoja na masharti mengine ya kiusalama yaliyowekwa na pande husika.

Hatua hiyo imekuja baada ya hali ya mvutano kuongezeka tena kufuatia mashambulizi ya Israel yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua tisa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano, huku Hezbollah ikijibu kwa kurusha makombora kuelekea kaskazini mwa Israel ambapo Matukio hayo yalikuwa jaribio kubwa kwa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Aprili mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Israel na Lebanon zimethibitisha tena kuwa mustakabali wa uhusiano wao unapaswa kuamuliwa na serikali zao huru bila kuingiliwa na mataifa mengine au makundi yasiyo ya kiserikali huku Makubaliano hayo pia yanajumuisha sharti la kuondolewa kwa wanajeshi wote wa Hezbollah kutoka eneo la kusini mwa Lebanon kati ya Mto Litani na mpaka unaodhibitiwa na Israel.

Pande hizo mbili zinatarajiwa kukutana tena Juni 22 kwa mazungumzo zaidi yenye lengo la kufikia makubaliano kamili ya kudumu. Hadi sasa, Hezbollah haijatoa tamko rasmi kuhusu makubaliano hayo, kabla ya tangazo hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema ana matumaini ya kuona mpango wa utekelezaji wa usalama nchini Lebanon ambao hautategemea kundi la Hezbollah.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here