Monday, 24 August 2026

WHO YAONYA BAADHI YA MATAIFA KUWEKA VIKWAZO VYA USAFIRI DRC

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuendelea kuwekwa kwa vikwazo vya jumla vya usafiri na baadhi ya mataifa kufuatia mlipuko unaoendelea wa virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), likisema hatua hizo zinadhoofisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema marufuku ya kusafiri iliyowekwa na […]

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuendelea kuwekwa kwa vikwazo vya jumla vya usafiri na baadhi ya mataifa kufuatia mlipuko unaoendelea wa virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), likisema hatua hizo zinadhoofisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema marufuku ya kusafiri iliyowekwa na zaidi ya nchi 12 imeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa shirika hilo kusambaza vifaa muhimu na kuratibu operesheni za kukabiliana na mlipuko huo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dkt. Tedros alisema kuwa vizuizi hivyo vinatatiza usafirishaji wa misaada na kuzuia mwitikio wa haraka unaohitajika ili kudhibiti kuenea kwa Ebola.

Onyo hilo linakuja baada ya Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia ya Canada kuthibitisha tena uamuzi wake wa kusitisha utoaji wa stakabadhi za uhamiaji kwa wakazi wa Congo, Uganda na Sudan Kusini kwa kipindi cha siku 90.

Mbali na Canada, nchi nyingine zikiwemo Marekani, Bahrain na Mexico zimeweka masharti au vizuizi vya usafiri kwa wasafiri kutoka maeneo yaliyoathirika na Ebola, Canada pia imeanzisha utaratibu wa karantini ya siku 21 kwa wasafiri wote wanaowasili kutoka Congo.

Wakati huo huo, WHO imesema inahitaji angalau dola milioni 115 katika miezi mitatu ijayo ili kuimarisha mapambano dhidi ya dharura hiyo ya kiafya ambapo shirika hilo limeeleza kuwa hadi sasa limefanikiwa kupata takribani asilimia 35 tu ya fedha zinazohitajika.

Hatahivyo WHO imezitaka nchi mbalimbali kuzingatia ushauri wa kitaalamu wa afya ya umma na kuepuka hatua zinazoweza kuathiri juhudi za kimataifa za kudhibiti mlipuko huo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *