Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amekutana na mwanazuoni na mhamasishaji wa dhana ya Utalii Halali duniani, Ismail Bullock, katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Zanzibar leo Juni 3, 2026.
Bullock aliwasili Ikulu kujitambulisha kwa Rais Mwinyi akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Samia Foundation, ambapo walijadili maendeleo na fursa za kukuza Utalii Halali nchini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Mwinyi alisifu mchango wa Bullock katika kutangaza na kuhamasisha Utalii Halali katika mataifa mbalimbali duniani, akisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono juhudi hizo kutokana na mchango wake katika kukuza sekta ya utalii inayozingatia misingi ya Kiislamu huku akionge kuwa Zanzibar itaendelea kujifunza kupitia mafunzo na uzoefu unaotolewa na wadau wa sekta hiyo ili kuhakikisha dhana ya Utalii Halali inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa taifa pamoja na wadau wa utalii.
Rais Mwinyi pia alimpongeza Bullock kwa juhudi zake za kuchapisha na kusambaza nakala za Qur’an Tukufu zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza, akieleza kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza uelewa kuhusu dhana ya Utalii Halali na mafundisho ya Kiislamu kwa jamii mbalimbali duniani.
Kwa upande wake, Bullock alisema lengo lake ni kuona dhana ya Utalii Halali inaeleweka na kutekelezwa kwa upana zaidi duniani, akibainisha kuwa tayari imeanza kupata umaarufu mkubwa katika nchi nyingi.
Kwa sasa, Bullock yupo Zanzibar akiendelea kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta ya utalii kuhusu namna ya kuendeleza na kutekeleza Utalii Halali ili kuongeza ushindani wa visiwa hivyo katika soko la kimataifa la utalii.
