Sunday, 11 October 2026

POLISI WABAINI MALI ZA WIZI JIJINI DAR ES SALAAM

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemtaja na kumkamata mtuhumiwa Abasi Kadewele maarufu kwa jina la Big Santiago kwa tuhuma za kupokea mali zinazodaiwa kuwa za wizi, ikiwa ni sehemu ya operesheni za kuimarisha usalama jijini humo. Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa Juni 3, 2026, mtuhumiwa huyo mkazi wa Msongola alikamatwa […]

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemtaja na kumkamata mtuhumiwa Abasi Kadewele maarufu kwa jina la Big Santiago kwa tuhuma za kupokea mali zinazodaiwa kuwa za wizi, ikiwa ni sehemu ya operesheni za kuimarisha usalama jijini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa Juni 3, 2026, mtuhumiwa huyo mkazi wa Msongola alikamatwa akiwa na simu janja 13 za aina mbalimbali, kompyuta mpakato mbili (laptop) na vifaa vitatu vya kuhifadhi taarifa (external drives), ambavyo vinadaiwa kuibwa kutoka maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam.

Polisi imesema kuwa katika mwezi Mei 2026, ilifanya operesheni mbalimbali zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wa makosa tofauti yakiwemo wizi, ubakaji, uvunjaji wa sheria za usalama barabarani na kupokea mali za wizi.

Katika upande wa usalama barabarani, madereva wanane walikamatwa baada ya kubainika kuwa na kiwango kikubwa cha kilevi. Kati yao, saba walikuwa madereva wa magari binafsi na mmoja alikuwa dereva wa gari la serikali. Wote wamechukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, jumla ya waendesha pikipiki 16,790 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani, ikiwemo kupita taa nyekundu, kutoheshimu vivuko vya waenda kwa miguu na kutovaa kofia ngumu. Kati yao, waendesha bodaboda 13,412 walikuwa wa pikipiki za magurudumu mawili huku 3,378 wakiwa wa pikipiki za magurudumu matatu.

Polisi pia imeeleza mafanikio ya kesi zilizofikishwa mahakamani, ambapo watuhumiwa watatu walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa makosa tofauti ikiwemo ubakaji na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kusaidia juhudi za kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama wa jamii.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *