Urusi imeendelea kukabiliana na mashambulizi mapya ya droni kutoka Ukraine baada ya kudungua droni kadhaa zilizokuwa zikielekea maeneo muhimu ya nchi hiyo, yakiwemo mkoa wa Leningrad na mji mkuu Moscow.
Kwa mujibu wa jeshi la Urusi, droni tatu zilidunguliwa katika mkoa wa Leningrad uliopo kaskazini-magharibi mwa nchi, saa chache kabla ya kuanza kwa Kongamano la Kimataifa la Uchumi la Saint Petersburg. Mkoa huo unatarajiwa kupokea viongozi wa kisiasa, wafanyabiashara na wageni kutoka mataifa mbalimbali katika mkutano huo wa kila mwaka.
Mji wa Saint Petersburg, ambao ni mwenyeji wa kongamano hilo na pia mji alikozaliwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, umeimarisha hatua za usalama kufuatia mashambulizi hayo.
Jeshi la Urusi limeongeza kuwa droni nyingine 13 zilizokuwa zikielekea Moscow zilidunguliwa alfajiri ya leo, hatua iliyosababisha usumbufu katika huduma za usafiri wa ndege na baadhi ya safari za treni.
Mashambulizi hayo ya Ukraine yanajiri saa chache baada ya Urusi kufanya mashambulizi makubwa ya makombora na droni dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv. Mashambulizi hayo yalifanyika kufuatia taarifa za vifo vya wanafunzi na raia kadhaa katika mkoa wa Luhansk.
Mapigano kati ya Urusi na Ukraine yanaendelea kushika kasi huku pande zote zikiongeza mashambulizi ya anga, jambo linalozidisha wasiwasi kuhusu usalama wa raia na miundombinu muhimu katika mataifa hayo mawili.
