Raia watano wa Msumbiji wameuawa nchini Afrika Kusini kufuatia wimbi jipya la mashambulizi yanayohusishwa na chuki dhidi ya wageni, huku hali ya usalama ikiendelea kuzua wasiwasi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Serikali ya Msumbiji imesema raia wake saba wamepoteza maisha nchini Afrika Kusini katika siku za karibuni, ambapo watano kati yao waliuawa na waandamanaji waliolenga wageni. Hata hivyo, polisi wa Afrika Kusini wamethibitisha vifo vya raia wawili wa Msumbiji pekee hadi sasa.
Ghasia hizo zilizuka mwishoni mwa wiki katika mji wa pwani wa Mossel Bay, ambapo waandamanaji waliteketeza kwa moto maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni, wengi wao wakitoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Maandamano dhidi ya wahamiaji wasiokuwa na vibali yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, hali iliyosababisha baadhi ya nchi za Afrika kuanza kuwaondoa raia wao kutoka Afrika Kusini. Ghana tayari imeanza kuwarejesha nyumbani zaidi ya raia 300, huku Nigeria nayo ikitangaza mipango ya kuchukua hatua kama hiyo.
Mauaji hayo yanatajwa kuwa ya kwanza kuripotiwa katika wimbi la sasa la ghasia zinazochochewa na chuki dhidi ya wageni, jambo linaloongeza hofu ya kurejea kwa vurugu zilizowahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka iliyopita.
Mamlaka za Afrika Kusini zimeendelea kufuatilia hali hiyo huku zikiahidi kuwachukulia hatua wahusika wa mashambulizi hayo.

