Waziri wa Ulinzi wa Bolivia amejiuzulu baada ya mwezi mzima wa maandamano makubwa yanayoikabili serikali ya Rais Rodrigo Paz, huku waandamanaji wakifunga barabara kuu zinazounganisha miji mikubwa nchini humo.
Kujiuzulu kwa waziri huyo kunamfanya kuwa mwanachama wa kwanza wa baraza la mawaziri la Paz kuondoka madarakani tangu serikali yake iingie madarakani mwezi Novemba mwaka jana. Serikali hiyo kwa sasa inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa makundi mbalimbali yanayotaka viongozi wake waondoke.
Rais Paz, ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kati, alichukua madaraka baada ya kumalizika kwa miongo miwili ya utawala wa vyama vya mrengo wa kushoto nchini Bolivia.
Maandamano hayo yanaongozwa na vyama vya wafanyakazi pamoja na makundi yanayomuunga mkono rais wa zamani Evo Morales. Waandamanaji wanapinga sera za serikali za kubana matumizi na kudai hatua zaidi zichukuliwe kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili wananchi.
Tangu mwezi Mei, waandamanaji wamekuwa wakizuia barabara muhimu zinazounganisha mji mkuu La Paz na mji wa El Alto, hali ambayo imeathiri usafiri na shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Serikali bado haijatangaza hatua mpya za kushughulikia mgogoro huo unaoendelea, huku shinikizo la kisiasa likiendelea kuongezeka.

