
Katika kuendelea kutekeleza kampeni ya Commit to Act 2026, Shirika la Road Safety Ambassadors of Tanzania (RSA Tanzania) hivi karibuni lilifanya ziara maalum katika Shule za Msingi Uzuri na Kilimani zilizopo Kata ya Manzese, Wilaya ya Kinondoni, kwa lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi, walimu na viongozi wa serikali za mitaa.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu, Habari na Mawasiliano wa RSA Tanzania, Ramadhani Msangi, pamoja na Afisa Tawala wa shirika hilo, Irene Msellem. Wajumbe hao waliungana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Salha Msonga, Mkuu wa Trafiki wa Wilaya ya Kipolisi ya Magomeni, ASP Alex Duguza, Msimamizi wa Kituo cha Urafiki, Inspekta Amina Said pamoja na viongozi wa serikali za mitaa.
Katika shule hizo mbili, wanafunzi walipatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara, namna salama ya kuvuka barabara, umuhimu wa kuzingatia alama za usalama na wajibu wao katika kujilinda dhidi ya ajali za barabarani. Mafunzo hayo yaliambatana na maonesho ya vitendo yaliyowawezesha wanafunzi kujifunza kwa karibu namna ya kutumia vifaa vya usalama wakati wa kuvuka barabara.
Kama sehemu ya kuimarisha usalama wa wanafunzi, RSA Tanzania iligawa fimbo maalum za kuvushia watoto barabarani (Junior Patrol Sticks) kwa shule zote mbili. Baada ya ugawaji huo, wanafunzi walipatiwa mafunzo ya namna ya kutumia vifaa hivyo kwa usahihi ili kusaidia kuvuka kwa usalama nyakati za kwenda na kutoka shuleni.
Walimu wa shule hizo walieleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema elimu pamoja na vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuongeza uelewa wa watoto kuhusu usalama barabarani.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Shule ya Msingi Kilimani, Mwalimu Mkuu Msaidizi Fatuma Dhahabu alisema shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 1,800 wakiwemo watoto wa chekechea na wenye mahitaji maalum, hali inayoongeza umuhimu wa kuwepo kwa mazingira salama ya kuwafikisha na kuwarejesha wanafunzi nyumbani.
Alisema pamoja na uwepo wa matuta katika eneo hilo, bado kuna changamoto kubwa kwa kuwa baadhi yake hayana alama zinazoonekana vizuri na nyingine zimefutika kutokana na matumizi ya muda mrefu. Kwa mujibu wake, hali hiyo inahatarisha usalama wa wanafunzi wanaovuka barabara kila siku.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Kilimani, Karimu Issa Mchelu, aliipongeza RSA Tanzania kwa kufika katika eneo hilo na kutoa elimu kwa wanafunzi, walimu na viongozi wa serikali za mitaa. Alisema ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye uelewa wa masuala ya usalama barabarani.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tupendane, Abdilahi Pazi, alisema wananchi wanathamini jitihada zilizofanywa na TARURA kwa kujenga matuta katika eneo hilo, lakini bado kuna changamoto ya zebra crossings zilizofutika na ukosefu wa taa za kuwasaidia wanafunzi kuvuka barabara kwa usalama.
Alieleza kuwa eneo hilo limewahi kushuhudia vifo vya wanafunzi wawili kutokana na ajali za barabarani, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuchukua hatua za haraka za kuboresha miundombinu ya usalama.
“Tunashukuru matuta yaliyowekwa, lakini tunahitaji yaongezwe ubora kwa kuwekwa alama zinazoonekana vizuri. Pia tunahitaji zebra crossings zichorwe upya na kuwepo kwa taa za kuvukia wanafunzi,” alisema.
Sauti kama hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Bodaboda Sinza Darajani, Ibrahim Said Nanga, ambaye alisema madereva wa bodaboda mara nyingi hulazimika kusimamisha shughuli zao za kila siku ili kuwasaidia wanafunzi kuvuka barabara kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki kwa watembea kwa miguu.
Alisema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakitoa maoni kuhusu umuhimu wa kuweka taa za kuongoza magari na watembea kwa miguu katika eneo hilo, lakini bado hatua hizo hazijatekelezwa.
Kwa mujibu wake, tuta lililopo kwa sasa lipo mbali na makutano ya barabara kiasi kwamba madereva wanapolivuka huongeza mwendo kabla ya kufika kwenye eneo ambalo wanafunzi na watembea kwa miguu huvuka.
“Tunahitaji matuta yawe karibu zaidi na makutano, zebra crossings ziwe wazi na zionekane, na ikiwezekana kuwe na kibanda cha askari wa usalama barabarani katika eneo hili,” alisema.
Aliongeza kuwa eneo hilo lina shule zaidi ya tatu, zahanati, nyumba za ibada na uwanja wa mpira, hali inayosababisha muingiliano mkubwa wa watumiaji wa barabara na kuongeza hatari ya ajali kwa watembea kwa miguu.
Kwa upande wao, maafisa wa Kikosi cha Usalama Barabarani walisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na kuahidi kuendelea kutembelea shule hizo mara kwa mara ili kuimarisha uelewa wa watoto kuhusu matumizi salama ya barabara.
Ziara hiyo imeonyesha wazi kuwa pamoja na elimu inayotolewa kwa watumiaji wa barabara, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha miundombinu ya usalama katika maeneo yanayozunguka shule ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kujifunzia na kukua.
Kupitia kampeni ya Commit to Act 2026, RSA Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha hatua za vitendo zitakazosaidia kupunguza ajali za barabarani na kulinda maisha ya watoto pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

