Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) imechagua jumla ya wanafunzi 246,197 kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa mwaka 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya zoezi la uchaguzi huo, Prof. Shemdoe amesema kati ya wanafunzi waliochaguliwa, wasichana ni 114,102 na wavulana ni 132,095, huku mchakato huo ukifanyika kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na mtaala ulioboreshwa.
Amesema wanafunzi 172,114 sawa na asilimia 69.9 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule za sekondari za Serikali 856 nchini, wakati wanafunzi 74,083 sawa na asilimia 30.1 wamechaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya ufundi.
Prof. Shemdoe amesema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza Julai 6, 2026, ambapo wanafunzi wanatakiwa kuanza kuripoti shuleni kuanzia Julai 4, 2026 na mwisho wa kuripoti utakuwa Julai 31, 2026.
Aidha, amesisitiza kuwa hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko ya shule kwa wanafunzi waliopangwa, akieleza kuwa nafasi zilizopo katika shule husika zimezingatiwa kikamilifu wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Ametoa wito kwa wanafunzi na wazazi kufuata ratiba iliyotolewa ili kuhakikisha wanafunzi wanaripoti kwa wakati na kuanza masomo yao kwa mujibu wa kalenda ya elimu ya Serikali.
Kujua wapi kijana wako amepangiwa, bonyeza kiungo hapa chini ukiwa na namba yake ya mtihani wa kidato cha nne
https://selform.tamisemi.go.tz/content/selection-and-allocation/

