Ufaransa imekamata meli ya mafuta iitwayo Tagor inayoshukiwa kuwa sehemu ya mtandao wa meli za Urusi zinazofanya kazi kwa njia za usiri au udanganyifu ili kusafirisha bidhaa zilizowekewa vikwazo vya kimataifa.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema operesheni hiyo ilifanyika kwa ushirikiano wa maafisa wa usalama na msaada wa Uingereza, ambapo helikopta ya kijeshi ilitumika kusaidia hatua ya ukaguzi na ukamataji.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za baharini, meli hiyo ilikamatwa katika Bahari ya Atlantiki ikiwa umbali wa takribani maili 400 za baharini magharibi mwa eneo la Brittany. Inadaiwa kuwa meli hiyo ilikuwa ikitumia bendera ya kughushi wakati wa operesheni hiyo, jambo linaloimarisha mashaka ya kuhusika kwake na kile kinachoitwa “shadow fleet” ya Urusi.
Akizungumza kupitia mtandao wa X, Macron alisema kuwa ni jambo lisilokubalika kwa meli kukwepa vikwazo vya kimataifa, kuvunja sheria za bahari na kufadhili vita vinavyoendelea nchini Urusi dhidi ya Ukraine.
Kwa upande wake, serikali ya Urusi kupitia msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, imelaani hatua hiyo ikieleza kuwa ukamataji huo ni “haramu” na kufananisha tukio hilo na kitendo cha uharamia wa kimataifa. Urusi imesema inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa mizigo yake ya kibiashara.
Meli ya Tagor ni ya nne kukaguliwa au kukamatwa na Ufaransa tangu Septemba 2025 ikiwa sehemu ya operesheni inayoendelea dhidi ya mtandao wa meli zinazodaiwa kukwepa vikwazo vya kimataifa.
