Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amewataka watendaji wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai kuendelea kujiimarisha kitaaluma na kutumia teknolojia za kisasa ili kukabiliana na changamoto za uhalifu wa kisasa unaotumia mbinu za hali ya juu.
Akifungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo watendaji wa kamisheni hiyo katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi, Juni 1, 2026, IGP Wambura alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadilisha namna uhalifu unavyotekelezwa, hivyo kuna haja ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa ushahidi.
Alieleza kuwa matumizi ya mbinu za kisayansi katika uchunguzi wa makosa ya jinai ni muhimu katika kusaidia upatikanaji wa haki kwa kuhakikisha ushahidi sahihi unapatikana na kutumika ipasavyo katika mifumo ya sheria.
IGP Wambura aliwapongeza watendaji wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kufika maeneo ya matukio, kukusanya ushahidi na kusaidia uchunguzi wa kisayansi. Alisisitiza kuwa hakuna uhalifu unaoweza kutendeka bila kuacha ushahidi unaoweza kuwasaidia wataalamu kuwabaini wahalifu
Aidha, amewataka watendaji hao kuzingatia weledi, uadilifu na kujifunza mara kwa mara ili kuimarisha utendaji wao na kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi pamoja na mfumo mzima wa haki jinai huku akisisitiza Jeshi la Polisi linaendelea kuwekeza katika mafunzo na teknolojia za kisasa ikiwemo uchunguzi wa vinasaba (DNA), uchambuzi wa kidigitali na mbinu nyingine za kisayansi ili kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao, uhalifu wa kimataifa na makosa mengine yanayohitaji uchunguzi wa kisasa.
“Ushahidi mnaokusanya una mchango mkubwa katika kuwapatia haki waathirika wa uhalifu, kuwawajibisha wahalifu na kujenga imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na mfumo wa haki jinai,” alisema IGP Wambura.
Aliongeza kuwa matarajio ya Jeshi la Polisi ni kuona maarifa yatakayopatikana katika kikao hicho yanatumika kuleta mabadiliko chanya katika utendaji wa watendaji wote wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai nchini.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi, Kamishna wa Polisi (CP) Shaban Hiki, alimshukuru IGP Wambura kwa kuendelea kuiwezesha kamisheni hiyo kupitia mafunzo na maboresho ya teknolojia yanayolenga kuongeza ufanisi katika uchunguzi wa makosa ya jinai.
