Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 108.02 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Dkt. Gwajima amesema fedha hizo zitatumika kuendeleza shughuli za maendeleo ya jamii, ustawi wa watoto, uwezeshaji wa wanawake, makundi maalum pamoja na wafanyabiashara ndogondogo nchini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara inatarajia pia kukusanya maduhuli ya shilingi bilioni 7.04 kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo ada za wanafunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, mauzo ya mitaala, ada za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na ada za vituo vya kulelea watoto.
Dkt. Gwajima amesema kati ya fedha zinazoombwa, shilingi bilioni 50.14 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida ya Wizara, ambapo shilingi bilioni 23.32 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na shilingi bilioni 26.82 kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji. Aidha, shilingi bilioni 57.89 zimetengwa kwa miradi ya maendeleo, ikiwemo shilingi bilioni 36.92 kutoka Serikali na shilingi bilioni 20.97 kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Katika hotuba hiyo, Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuimarisha malezi, ulinzi na ustawi wa watoto kupitia programu mbalimbali zinazolenga kujenga kizazi chenye maadili, afya bora na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa. Amesisitiza kuwa watoto ni rasilimali muhimu na mtaji wa Taifa unaohitaji kulindwa na kuendelezwa ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumzia masuala ya ustawi wa watoto, Dkt. Gwajima amesema Wizara imepokea jumla ya mashauri 19,425 ya matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa. Kati ya mashauri hayo, 3,500 yalipelekwa mahakamani huku mashauri 15,925 yakiendelea kushughulikiwa na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Kwa upande wa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, Waziri huyo amesema takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa matukio ya ukatili wa kingono kwa jinsia zote yamepungua kutoka matukio 12,749 mwaka 2024 hadi matukio 11,625 mwaka 2025.
Hata hivyo, ameonya kuhusu ongezeko la changamoto zinazotokana na matumizi ya teknolojia kwa watoto, akibainisha kuwa tafiti zinaonesha asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 hutumia simu janja, huku asilimia 4 kati yao wakikumbana na aina mbalimbali za ukatili mtandaoni.
Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto na kuhamasisha matumizi salama ya mitandao ya kijamii ili kukabiliana na vitendo vya ukatili na kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye ustawi.
