Maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameeleza kufurahishwa na kupona kwa wagonjwa watano waliokuwa wameambukizwa aina nadra ya virusi vya Ebola vya Bundibugyo, hatua inayotajwa kuwa mafanikio muhimu katika mapambano dhidi ya mlipuko unaoendelea mashariki mwa nchi.
Wagonjwa wanne, ambao ni wauguzi waliopata maambukizi wakati wakiwahudumia wagonjwa wa Ebola, wameruhusiwa kurejea nyumbani katika mji wa Bunia, makao makuu ya mkoa wa Ituri. Hii imeongeza idadi ya waliopona ugonjwa huo kufikia watano, baada ya mfanyakazi mmoja wa maabara kuruhusiwa kutoka hospitalini siku ya Ijumaa.
Walionusurika hao waliondoka katika kituo cha matibabu cha Bunia jana na kueleza shukrani zao kwa kuendelea kuwa hai licha ya hatari kubwa ya ugonjwa huo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Umma nchini DRC, Dk. Mwamba Kazadi, amesema kupona kwa wagonjwa hao ni ushindi mkubwa unaostahili kusherehekewa. Amesema mafanikio hayo yametokana na ugunduzi wa mapema wa maambukizi na huduma thabiti za matibabu zilizotolewa kwa wagonjwa.
Mlipuko wa sasa unasababishwa na spishi ya Ebola ya Bundibugyo, ambayo hadi sasa haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa rasmi.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ambaye yuko katika ziara ya mkoa wa Ituri, amesema ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika kudhibiti ugonjwa huo Amewataka wananchi kushirikiana na wahudumu wa afya baada ya baadhi ya wakazi kushambulia vituo vya matibabu kutokana na kutoridhishwa na taratibu kali za mazishi zinazokinzana na mila za wenyeji.
Mbali na Ituri, maambukizi ya Ebola yameripotiwa pia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa DRC, pamoja na nchini Uganda hukuTaarifa zinaonyesha kuwa takribani watu 246 wamefariki dunia kutokana na mlipuko huo, huku zaidi ya watu 1,000 wakishukiwa kuambukizwa virusi vya Ebola. Nchini Uganda, mamlaka za afya zimeripoti kifo kimoja na kuthibitisha maambukizi ya watu tisa hadi sasa.
