Tuesday, 25 August 2026

GALANOSI YAENDELEA KUFANYA VYEMA UFAULU MASOMO YA SAYANSI

SHULE ya Sekondari ya Wavulana ya Galanos iliyopo mkoani Tanga, imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, huku matokeo ya mitihani ya kitaifa yakionyesha ongezeko la ufaulu na ushindani mkubwa katika masomo ya sayansi. Akizungumza Mei 31,2026, Mkuu wa shule hiyo, Amos Sembe, amesema Galanos ilianzishwa mwaka 1964 ikiwa shule maalumu ya masomo ya kilimo, lakini baadaye ilipanua […]

SHULE ya Sekondari ya Wavulana ya Galanos iliyopo mkoani Tanga, imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, huku matokeo ya mitihani ya kitaifa yakionyesha ongezeko la ufaulu na ushindani mkubwa katika masomo ya sayansi.

Akizungumza Mei 31,2026, Mkuu wa shule hiyo, Amos Sembe, amesema Galanos ilianzishwa mwaka 1964 ikiwa shule maalumu ya masomo ya kilimo, lakini baadaye ilipanua wigo wake na sasa inatoa tahasusi saba katika masomo ya sayansi, biashara na sanaa kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita

Amesema shule hiyo yenye walimu 42 na wanafunzi 924 ni miongoni mwa wanufaika wa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP), ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa mujibu wa Sembe, mradi huo umeiwezesha shule kupata vifaa vya TEHAMA na maabara, pamoja na kuwajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu na zana za kisasa katika ufundishaji.

Amesema hatua hiyo imeongeza hamasa na ushindani wa wanafunzi katika masomo ya sayansi, huku wanafunzi wa tahasusi za sanaa na biashara wakionyesha ari kubwa ya kujifunza masomo hayo.

“SEQUIP imeleta mabadiliko makubwa katika shule yetu. Walimu wamepata mafunzo ya kitaalamu ambayo hapo awali yalikuwa nadra kutokana na mabadiliko ya mitaala. Sasa uwezo wao wa kufundisha umeongezeka na matokeo yanaonekana wazi,” amesema .

Akitolea mfano wa mafanikio hayo, Sembe alisema katika mitihani ya mwaka 2025, wanafunzi wote 71 wa somo la fizikia, waliofanya mtihani walifaulu. Pia katika somo la Hisabati, wanafunzi wote 135 waliofanya mtihani walifaulu.

Hata hivyo, amesema somo la Kemia bado linahitaji kuimarishwa zaidi kutokana na changamoto ya wanafunzi kutopata nafasi ya kutosha kufanya mazoezi ya vitendo mara kwa mara.

Kwa upande wa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita wa mwaka jana, amesema kati ya wanafunzi 456 waliofanya mtihani, wanafunzi 252 walipata Daraja la Kwanza, 158 Daraja la Pili na 54 Daraja la Tatu, ikidhihirika kuendelea kuimarika kwa kiwango cha ufaulu shuleni hapo.

Kutokana na mafanikio hayo, Sembe ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha mradi wa SEQUIP unaendelea ili kuendeleza maboresho yaliyopo na kuongeza ufaulu wa masomo ya sayansi na hisabati nchini.

Amesema pamoja na shule kunufaika na vifaa mbalimbali vya maabara, bado kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya kisasa vya maabara na TEHAMA vinavyoweza kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.

Naye Mwalimu wa Biolojia katika shule hiyo, James Likiliwike, amesema mafunzo aliyopata kupitia SEQUIP mwaka jana yamemsaidia kupata mbinu mpya za ufundishaji, matumizi ya TEHAMA na namna ya kutumia zana zinazopatikana kwenye mazingira yanayomzunguka ili mwanafunzi kujifunza.

Amesema maarifa hayo yalimwezesha kuwa mwalimu mwenye ufanisi zaidi, anayewasaidia wanafunzi kuelewa masomo kwa urahisi na kuyapenda kuliko ilivyokuwa awali.

“Mbinu hizi zimeongeza ushiriki wa wanafunzi darasani na zimeimarisha uelewa wao wa somo. Tuna matarajio makubwa ya kufanya vizuri zaidi katika mitihani ijayo,” amesema .

Mradi wa SEQUIP umekuwa kichocheo muhimu cha maboresho katika sekta ya elimu ya sekondari nchini kwa kuimarisha uwezo wa walimu, miundombinu ya kujifunzia na matokeo ya wanafunzi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *