Tuesday, 25 August 2026

POLISI NIGERIA WATAHADHARISHA MASHAMBULIZI YA KULIPIZA KISASI KUFUATIA MVUTANO AFRIKA KUSINI

Polisi nchini Nigeria wamewataka wananchi kujiepusha na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia na biashara za Afrika Kusini kufuatia taarifa za mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni yanayodaiwa kuwalenga Wanigeria wanaoishi nchini humo. Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi la Nigeria, Anthony Okon Placid, amesema vyombo vya usalama vimefanya tathmini ya […]

Polisi nchini Nigeria wamewataka wananchi kujiepusha na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia na biashara za Afrika Kusini kufuatia taarifa za mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni yanayodaiwa kuwalenga Wanigeria wanaoishi nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi la Nigeria, Anthony Okon Placid, amesema vyombo vya usalama vimefanya tathmini ya hali hiyo baada ya mkutano ulioongozwa na mshauri wa usalama wa taifa. Amehakikishia wananchi kuwa hakuna sababu ya kuwa na hofu kwani serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya tukio hilo.

Placid amesema mamlaka za Nigeria zinaendelea kushirikiana na serikali ya Afrika Kusini pamoja na wadau wengine wa kimataifa kupitia njia za kidiplomasia na kiusalama ili kuhakikisha usalama wa raia wa Nigeria walioko nchini humo.

Amesisitiza kuwa licha ya wasiwasi uliopo kuhusu mashambulizi dhidi ya Wanigeria nchini Afrika Kusini, wananchi hawapaswi kuchukua sheria mkononi mwao kwa kufanya vitendo vya kulipiza kisasi.

“Ingawa wasiwasi kuhusu mashambulizi dhidi ya Wanigeria nchini Afrika Kusini unaeleweka, wananchi wanashauriwa kutokuchukua sheria mikononi mwao. Mashambulizi ya kulipiza kisasi, vurugu, vitisho, uharibifu wa mali, matamshi ya chuki au vitendo vyovyote vinavyotishia amani ya umma na usalama wa taifa ni kinyume cha sheria na havitavumiliwa,” amesema Placid.

Polisi pia wameeleza kuwa hatua za ziada za kiusalama zimeimarishwa katika balozi na misheni za kigeni, miundombinu muhimu pamoja na maeneo mengine nyeti nchini humo ili kuzuia matukio yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama.

Onyo hilo linakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka nchini Afrika Kusini kufuatia maandamano yanayolenga wahamiaji. Waandamanaji wamekuwa wakidai kuwa wahamiaji wasiokuwa na stakabadhi halali wanaongeza shinikizo kwenye huduma za umma na wametoa wito kwa serikali kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *