
Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Hayati Dk. John Magufuli alimshawishi mwaka 2015 kuendelea na siasa baada ya kutangaza kustaafu kugombea ubunge wa Jimbo la Songea.
Akizungumza leo katika Misa ya kumuombea Hayati Susana Magufuli mjini Chato, Dk. Nchimbi amesema Magufuli alipinga uamuzi wake wa kustaafu na hata kumwambia yupo tayari kumpa nafasi ya ubunge, lakini alikataa.
Amesema baada ya mwaka mmoja, Magufuli alimtafuta tena na baadaye akamteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil.
Dk. Nchimbi amesema watu wengi walimwona Magufuli kama mtu mkali, lakini kwake alikuwa mtu mwenye kujali na anayependa kuona watu wanafanikiwa.
“Aliniambia, ‘Siwezi kuharibu ndoto yako, wewe bado ni kijana,’” amesema Dk. Nchimbi huku akieleza kuwa maneno hayo bado yanamuongoza katika maisha yake ya uongozi.
