LONDON, Uingereza
MSIMU huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umeingia hatua ngumu ya nusu fainali, zikiwa zimebaki timu nne zinazowania nafasi mbili za kucheza fainali.
Atletico Madrid, baada ya kuiondosha Barcelona kwa kichapo cha jumla ya mabao 3-2, sasa ina kibarua cha kuikabili Arsenal.
Bayern Munich, ambayo imeing’oa Real Madrid kwa kipigo cha jumla ya mabao 6-4, itavaana na PSG iliyoing’oa Liverpool kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-0.
BAYERN V PSG
PSG ni mabingwa watetezi lakini watakutana na moja ya timu zilizo na ubora wa hali ya juu msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.
Nusu fainali ya kwanza itachezwa kati ya Aprili 28-29, kabla ya timu hizo kurudiana mjini Munich wiki moja baadaye.
Katika miaka 10 ya hivi karibuni, vigogo hao wamekutana mara 8 lakini PSG imeshinda mechi mbili pekee.
Mara ya mwisho kwa PSG na Bayern kuvaana ilikuwa robo fainali ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu mwaka jana, ambapo wakali hao wa Paris walishinda na kwenda nusu fainali.
Safari hii, Bayern Iko moto kutokana na viwango bora vya Michael Olise, Harry Kane na Luis Diaz, wakati jeuri ya PSG iko kwa Ousmane Dembele, Khvicha Kvaratskhelia na Vitinha.
ATLETICO V ARSENAL
Kwa Atletico, hii ni mara yao ya kwanza kufika nusu fainali tangu mwaka 2017 na wanasaka ubingwa wao wa kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa.
Arsenal wao wameingia nusu fainali kwa msimu wa pili mfululizo na wana historia nzuri ya kuifunga Atletico mabao 4-0 pale Emirates katika mchezo wa Oktoba, 2025.
Hata hivyo, kocha Diego Simeone hajasahau kuwa Atletico ilitandikwa mabao 4-0 na Arsenal katika hatua ya makundi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, matokeo hao ni kabla ya kocha Diego Simeone kumsajili Ademola Lookman, ambaye ametengeneza kombinesheni hatari ya ushambuliaji akishirikiana na Antoine Griezmann na Julian Alvarez.
Imeandaliwa na Hassan Mwasha






