Timu ya Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanya ziara maalum ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya jiji hilo.
Ziara hiyo imelenga kujionea hali halisi ya maendeleo ya miradi pamoja na kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara, ambapo timu ilikagua maendeleo ya barabara ya Eso Long Dong pamoja na barabara nyingine zinazoendelea kuboreshwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Pia, timu imekagua miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya katika shule mbalimbali, hususan katika eneo la Kalimaji, ikiwa ni jitihada za kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Aidha, timu hiyo imetembelea na kukagua miradi ya ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya, ambapo lengo ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo hivyo. Miradi hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Halmashauri katika kuboresha ustawi wa jamii kupitia sekta muhimu kama afya na elimu.
Kwa ujumla, timu imeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, huku ikitoa maelekezo machache ya kuboresha pale ilipoonekana kuna changamoto ndogo ambapo imesisitiza kuwa miradi yote iliyotembelewa na kukaguliwa inaendeshwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, jambo linaloonesha uwajibikaji, ubunifu na uwezo wa kujitegemea katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo bila kutegemea kwa kiasi kikubwa misaada ya nje.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika ipasavyo na miradi inakamilika kwa wakati na kwa manufaa ya wananchi wote wa Jiji la Arusha.







