RIPOTA PANORAMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko kesho anatarajiwa kuweka jiwe na msingi katika mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme lililopo Mto Malagarasi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Nishati, Neema Mbuja, mradi huo utazalisha megawati 49.5.
Taarifa ya Mbuja inaeleza kuwa ujenzi utahusisha njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132, kutoka Igamba hadi Kidahwe yenye urefu wa kilomita 54 na kituo cha kupoza na kusambaza umeme, msongo wa kilovoti 400/220/132/33 cha Kidahwe mkoani Kigoma.
Mbuja anaandika katika taarifa hiyo kuwa mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 144.14 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 338 ambapo Serikali itatoa Dola za Marekani milioni 4.14 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itatoa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 140.
āMradi utahusisha sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni ujenzi wa bwana la kuzalisha umeme ikiwemo tuta, njia za kupitisha maji, jumba la mitambo ya kufua umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 49.5 na kituo cha kupokea umeme na kuuongezea nguvu wa msongo wa kilovoti 132.
āSehemu ya pili ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 54 ambayo itaunganisha kituo cha kuzalisha umeme na Gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe,ā inasomeka taarifa hiyo.
Mbuja anaeleza zaidi kuwa sehemu ya tatu ni ujenzi wa mtandao wa usambazaji umeme katika vijiji saba vinavyopitiwa na mradi na ambavyo ni Mizungwe, Kidahwe, Mwamila, Kalenge, Kazuramimba, Mlela na Igamba.
Taarifa inaeleza kuwa mradi wa Mto Malagarasi unatarajiwa kuzalisha umeme wa wastani wa Gigawati hour 181 kwa mwaka utakaotumika ndani ya Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani.