RIPOTA MAALUMU
Moshi
SHIRIKA Lisilo la Kiserikali la Mema Foundation limekata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi kuhusu umiliki na uingizwaji wa vifaa tiba vya kupimia macho.
Vifaa tiba hivyo viliingizwa nchini kutoka Denmark vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 92,870.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu uamuzi wa kukata rufaa, Katibu Mkuu wa Mema Foundation, Alfred Kaaya amesema hajawaridhishwa na uamuzi uliotolewa na Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi katika kesi namba 7 ya mwaka 2022 ya kupinga kunyangāanywa umiliki wa vifaa tiba hivyo.
Kaaya amesema, katika hukumu hiyo ambayo wanaikatia rufaa, Jaji Simfukwe aliainisha kuwa mlalamikaji (Kaaya) katika ushahidi wake alishindwa kuishawishi mahakama kwamba taasisi yake ndiyo mmiliki wa vifaa tiba hivyo.
Katika kesi hiyo, Shirika la Mema Foundation kupitia kwa Katibu Mkuu, Kaaya liliwafungulia kesi ya madai Charlotte Srandfelt, Dk. Focus Maro, Shirika Lisilo la Kiserikali la Good Samaritan Foundation na Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa kuchukua vifaa hivyo bila idhini ya Mema Foundation na kukiuka makubaliano ya kimkataba.
Katika madai yake, Kaaya alidai kuwa akiwa Katibu Mkuu wa Shirika la Mema Foundation ndiye aliyeandaa nyaraka zote za kuingiza vifaa hivyo ambapo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) walifanya ukaguzi na kutoa kibali namba TMDA-WEB0021/MDR/SIPER/5988 na Mamlaka ya Mapato (TRA) walitoa barua na kibali cha msamaha wa kodi.
Kaaya alidai kuwa alipokea vifaa tiba hivyo akiwa na mdaiwa wa kwanza, Charlotte Strandfelt ambaye awali alikuwa mshirika wake katika shirika la Mema Foundation na kwamba baada ya kuvichukua walivipelekaa katika hoteli inayofahamika kwa jina la Pazuri iliyoko nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Alidai kuwa baadaye katika mazingira ya kutatatanisha na yasiyoeleweka, vifaa tiba hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, ambako Mkurugenzi Mkuu, Profesa Giliard Masenga alikiri kuvipokea kwa barua yenye kumbukumbu namba KCMC/A.43/VOL1X/48.
Vifaa tiba hivyo viliingizwa nchini Novemba, 2021 kutoka nchini Denmark na vilikuwa msaada kutoka Shirika Lisilo la Kiserikali la Better Vision Africa la Denmark.
Vilipaswa kugawiwa bure kwa wahitaji/wagonjwa hasa wenye ulemavu wa ngozi, watoto na wazee katika baadhi za wilaya za Mkoa wa Arusha na vilipata msahama wa kodi unaokadiriwa kuwa Shilingi milioni 42, kutoka TRA.
MSINGI WA RUFAA
Kwa mujibu wa Kaaya, taasisi yake inapinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda Moshi kwa wadaiwa namba 1, 2, 3 na 4 kuwa katika kesi hiyo walishindwa kuwasilisha kielelezo chochote cha nyaraka mahakamani inayothibitisha kuwa wao ni wamiliki na ndiyo walioingiza vifaa hivyo nchini kama inavyokubalika kisheria.
āKwamba Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi haikuangalia umuhimu wa mamlaka za Serikali zinazohusika na msamaha wa kodi (TRA/TMDA) kufika mahakamani au kuwasilisha ushahidi wa maandishi ili kuithibitishia mahakama umiliki na uhalali wa vifaa tiba hivyo,ā kinasomeka kipengele kimoja kwenye cha rufaa hiyo.
Kaaya anasema Mahakama Kuu, Kanda Moshi ilishindwa kungāamua pale wajibu rufaa namba 1 na 2 waliposhindwa kutaja mbele ya mahakama idadi ya makasha yenye vifaa walivyopokea na kuviweka chini ya himaya yao.
Kwamba Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi ilipotoka kisheria kuendelea na shauri hilo bila kuzingatia wadaiwa namba 1, 2, 3 na 4 hawakuwasilisha ushahidi wa kimaandishi mbele ya mahakama kama sheria inavyoelekeza.
Akizungumza hilo, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Profesa Gileard Masenga alithibitisha kuwepo mgogoro kuhusu vifaa tiba hivyo na kuongeza kuwa hospitali yake ndiyo iliyopewa dhamana ya kuviingiza nchini.
Hata hivyo alipoulizwa kuhusu nani aliyepewa nyaraka za msamaha wa kodi na TRA, Profesa huyo alishindwa kutoa majibu na badala yake alisema vifaa tiba hivyo vipo hapo hosptalini na wanasubiri maelekezo ya mmiliki wake.
āVifaa vipo hapa hospitali, tunasubiri maelekezo ya mmiliki wakeā alisema Profesa Masenga.
Shirika Lisilo la Kiserikali la Mema Foundation lenye makao yake Usariver, Wilaya ya Arumeru lilisajiliwa kisheria Agosti 10, 2021 na kupewa namba ya usajili ooNGO/2076.