RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imepanga kutumia Shilingi bil. 787 kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu 250,000 wakiwemo 80,000 wa shahada ya kwanza kwa mwaka 2024/2025.
Mpango huo wa serikali umeelezwa leo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 15 wa Bunge, Dodoma.
“Maandalizi ya awali yameanza ikiwa ni pamoja na kusambaza mwongozo wa upangaji na utoaji mikopo, kufungua dirisha la uombaji mikopo kwa mwaka 2024/2025 kwa muda wa siku 90 kuanzia tarehe 1 Juni hadi 31 Agosti, 2024 na kutoa elimu kwa waombaji mkopo na wadau wengine,” amesema.
Majaliwa amesema mwaka wa fedha 2023/2024, serikali ilitoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu 224,056 na hadi Juni, 2024 wanafunzi walikuwa wamepatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bil 743.2, sawa na asilimia 94.6 ya fedha zilizotengwa.
Amesema mikopo hiyo ilitengwa kwa ajili ya wanafunzi wa ngazi ya stashahada, shahada ya awali, stashahada ya juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo, shahada za umahiri na uzamivu na ufadhili wa Samia (Samia Scholarships) katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.
Kuhusu urejeshaji mikopo hiyo, Majaliwa amesema Bodi ya Mikopo imeendelea kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika wa mikopo.
“Kwa mwaka 2023/2024, serikali ilipanga kukusanya Shilingi bil 230, hadi Mei 2024, Shilingi bil 161 zilikusanywa, sawa na asilimia 70 ya lengo,” alisema.
Akizungumza kuhusu kuimarisha ukusanyaji wa mikopo, Majaliwa amesema serikali imeweka mikakati kadhaa, ikiwemo kuwakumbusha waajiri kuwasilisha majina ya wanufaika ndani ya siku 28 baada ya kuwaajiri, kushirikiana na kuunganisha mifumo na wadau wa kimkakati kama vile NIDA, TRA na taasisi binafsi za ndani na nje ya nchi;
Pia kufanya kampeni za kuwafichua wanufaika, kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii na kufanya kaguzi kila mwezi kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi.
Wakati huo huo, amesema utaratibu wa mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, tayari serikali imekamilisha maandalizi ya uratibu wa upelekaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda kwenye mfuko wa mikopo ya vikundi na kusimamia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa miaka ya nyuma.
“Itakumbukwa kwamba mwezi Aprili 2023, serikali ilisitisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2023/2024, serikali imekamilisha maandalizi ya uratibu wa upelekaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 katika mamlaka za serikali za mitaa kwenda kwenye mfuko wa mikopo ya vikundi na kusimamia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa miaka ya nyuma.”
Majaliwa amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025, serikali imepanga kutoa mikopo ya Shilingi bilioni 228 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 63.7 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa Aprili, mwaka jana; Shilingi bil 63.2 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na Shilingi bil 101.1 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/2025.
Akitoa, amesema serikali imepanga utaratibu wa kutumia benki kwa Halmashauri 10 za majaribio ambazo ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa za Kigoma Ujiji na Songea, Miji ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.
Amesema, Halmashauri 174 zilizobaki zitatumia utaratibu ulioboreshwa ikiwemo uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na Kata.