Sunday, 11 October 2026

SERIKALI YATOA TAMKO MKUTANO WA SHIRIKA LA MAKAZI DUNIANI

RIPOTA PANORAMA Nairobi, Kenya SERIKALI imesema kuwa imeongeza kasi ya kuboresha miundombinu, makazi na huduma za jamii kwenye maeneo ya mijini na vijijini ili kuwawezesha watu wote kuishi katika makazi bora na salama. Hayo yamesemwa leo Jijini Nairobi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, kwenye Mkutano wa Shirika la […]

RIPOTA PANORAMA

Nairobi, Kenya

SERIKALI imesema kuwa imeongeza kasi ya kuboresha miundombinu, makazi na huduma za jamii kwenye maeneo ya mijini na vijijini ili kuwawezesha watu wote kuishi katika makazi bora na salama.

Hayo yamesemwa leo Jijini Nairobi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, kwenye Mkutano wa Shirika la Makazi Duniani unaoendelea jijini humo.

Akitoa tamko la nchi kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani ulioanza jana Jijini Nairobi, ambao kauli mbiu yake ni “hatma ya miji endelevu kupitia

ushirikishwaji na uwepo wa mifumo ya mahusiano ya kimataifa,” Waziri Mabula amesema Serikali ya Tanzania inachukua hatua madhubuti kukabiliana na ongezeko kubwa la watu mijini na changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi, kama sehemu ya malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals) ambayo kila nchi duniani inatekeleza.

Amesema kuwa takwimu za sensa ya watu na makazi nchini iliyofanyika mwaka 2022 zinaonyesha kuwa asilimia 35 ya Watanzania wanaishi mijini huku kukiwa na ongezeko la uhamiaji mijini la asilimia 4.8 kila mwaka kati ya Watanzania wote 61.7 milioni.

Waziri Mabula pia ameueleza mkutano huo kuwa Serikali inalenga kuendelea kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kuhamasisha matumizi ya usafiri usioharibu mazingira, kudhibiti mafuriko, kuweka mipango ya kuifanya miji iwe salama kwa mazingira na kuweka mipango ya kudhibiti kina cha bahari kisizidi na kuingia nchi kavu.

Sambamba na mipango hiyo amesema Serikali itaendelea kuhimiza matumizi bora ya uzalishaji nishati safi na endelevu.

Aidha, aliufahamisha mkutano huo kuwa Serikali imerasimisha makazi kwa asilimia 61 ya makazi yasiyopangwa nchini ambayo kwa sasa yametimia 3,400.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula akiwa katika Mashauriano na Waziri wa Nyumba na Makazi wa Venezuela, Ildemaro Arismande, Jijini Nairobi Kenya, leo.

Akasisitiza kuwa yote hiyo aliyoitaja ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya Taifa chini ya makubaliano ya Paris na kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochochewa kwa kiasi kikubwa na idadi kubwa ya watu kuhamia mijini na kwamba gharama zake haziwezi kuondolewa na Serikali peke yake.

Amesema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania inahitaji kiasi cha Dola za Marekani bilioni 19 hadi kufikia mwaka 2030 kwa maeneo ya kutekeleza mipango mbalimbali ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wajumbe wa Mkutano huo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika (Africa Food Systems Summit), AGRAF unaotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 4 mpaka 6 mwaka huu.

Wakati huo huo, Waziri Mabula amekutana na ujumbe kutoka nchi ya Venezuela ambao katika kikao hicho kilichoitishwa na Waziri wa Nyumba na Makazi wa nchi hiyo, Ildemaro Moises Arismandi, masuala mbalimbali yanayohusiana na nyumba, makazi na mipango miji yamezungumzwa. 

Sehemu wa wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Shirika la Makazi Duniani unaoendelea Jijini Nairobi Kenya

Waziri huyo wa Venezuela alikumbushia maombi ya nchi yake waliyowasilisha nchini Tanzania ya kufungua Ubalozi Jijini Dodoma. 

Akijibu maombi yao, Waziri Mabula aliuambia ujumbe huo kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anakaribisha mahusiano ya kimataifa ili kusaidia maendeleo ya watu na kwamba Serikali ya Tanzania imetenga eneo Jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga ofisi za Balozi mbalimbali katika eneo la mji wa Serikali.

Alisema kuwa Serikali ya Tanzania inakaribisha wawekezaji katika sekta ya nyumba na makazi ambao watasaidia kuharakisha upatikanaji wa nyumba bora kwa watanzania na kuboresha miji.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *