RIPOTA PANORAMA
BODI ya Bima ya Amana inachungulia shimoni wakati huu utendaji kazi wake ukiwa chini ya uwiano unaohitajika wa ukubwa wa mfuko kwa jumla ya amana zenye bima.
Bodi hiyo ya Bima ya Amana kwa sasa ina uwiano wa asilimia 3.31 ambacho ni kiwango cha chini kinachoathiri mchango wa bodi kwenye mtangamano wa kifedha nchini.
Hayo yamebainishwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2021/22.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Bodi ya Bima ya Amana haina mpango madhubuti wa ukusanyaji mikopo, ina matumizi makubwa kuliko mapato na ina wafanyakazi wasiozingatia ufanisi wa kazi zao.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Bodi ya Bima ya Amana inatakiwa kufikisha uwiano wa asilimia 20 kama ilivyokubaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ifikapo 2025 ili kuwalinda vya kutosha wenye amana endapo benki zitafilisika.
Inaeleza kuwa Bodi ya Bima ya Amana ina mpango usioridhisha wa ukusanyaji mikopo, pamoja na kukabiliwa na jukumu kubwa la kukusanya mikopo kutoka benki saba zilizofilisika.
“Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi iliweza kukusanya Shilingi bilioni 47.12 tu kati ya Shilingi bilioni 206.59 zilizotarajiwa kukusanywa kutoka katika benki saba zilizofilisika ambayo ni asilimia 23.
“Upungufu huu unapunguza uwezo wa Bodi ya Bima ya Amana wa kutathmini na kufuatilia shughuli za usanyaji,” anaeleza CAG katika ripoti yake.
Aidha ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa Bodi ya Bima ya Amana imetumia ghamara kubwa zinazohusu ufilisi wa benki saba zilizofilisika zinazofikia Shilingi bilioni 5.12 huku makusanyo ya madeni yakiwa Shilingi bilioni 5.30.
“Gharama kubwa zinazohusu ufilisi wa benki saba zilizofikia Shilingi bilioni 5.12 huku kukiwa na wasiwasi wa maslahi ya wadau kutolipwa ipasavyo kwa sababu makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 5.30.
“Hivyo kiasi kikubwa cha fedha iliyokusanywa kilitumika kama gharama za kazi ya kukusanyia mikopo hiyo,” anaeleza CAG.
Ripoti inaeleza zaidi kuwa Bodi ya Bima ya Amana inapaswa kusimamia na kupunguza gharama za ufilisi ziwe kwenye viwango vinavyokubalika na pia iangalie uwezekano wa kutumia mawakala wa kukusanya madeni ambao watalipwa kulingana na ufanisi wa kazi badala ya kuajiri wafanyakazi wa kudumu wanaolipwa mishahara bila kuzingatia ufanisi wao.
CAG anapendekeza Bodi ya Bima ya Amana kuandaa mpango kazi wenye malengo na muda maalumu wa kukusanya mikopo na kuwezesha kuuzwa kwa mali za benki zilizofilisika.
Pia anapendekeza kwa bodi hiyo kuchukua hatua za haraka kushughulikia upungufu alioubainisha kwenye ripoti yake na kuhahakisha maslahi ya wenye amana yanalindwa ipasavyo.
