KESI YA UNGA YA MUNA NA HARIRI MBELE YA GACACA

0
196

CHARLES MULLINDA

KESI ya unga. Watuma maombi kwa niaba ya serikali ni wachokonozi; na wajibu maombi ni, mosi; shahidi wa Serikali ambaye ushahidi wake mahakamani ulikinzana na wa mashahidi wenzake, pili; Muna, sasa ianze upya katika Mahakama ya kienyeji ya Gacaca.

Mahakama ya Gacaca ianze kupitia upya mwenendo wa kesi dhidi ya washindi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mohamedi Hariri na mkewe Muna Saidi waliokuwa wakishtakiwa kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gram 214.11 ili kuondoa minong’ono isiyopendeza kuisikia.

Hariri na Muna walishinda kesi ya kukutwa na unga baada ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ambao ni Serikali kuwa ulishindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka yoyote.

Haya ni ya mahakama kuu, tuyaache kwa sababu hatuna mamlaka nayo isipokuwa tu kuyatumia kama kesi darasa. Kwa sababu hiyo, tuyabebe sasa twende nayo Mahakama ya Gacaca tukaanze upya kuupitia mwenendo wa kesi hii baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Mchokonozi katika Magereza ya Segerea na Keko ambako kuna mameja wa kike warembo wenye ukarimu wa hali ya juu.

Twendeni Gacaca na maombi ya kupitia upya mwenendo wa kesi tukianza na shahidi wa Serikali ambaye wakati makachero wakielekea nyumbani kwa Muna na Hariri huko Kinondoni kufanya upekuzi, kabla ya kuanza upekuzi walimualika awe shuhuda na yeye akaitikia wito akawepo, akashuhudia tukio zima.

Tuiombe Mahakama ya Gacaca ipitie kabrasha la shahidi huyo na ijiridhishe kama kweli alikuwepo wakati wa upekuzi, akashuhudia kilichokamatwa na kutia sahihi yake katika hati ya upekuzi kuthibitisha kuwa kweli ameshuhudia kukamatwa kwa mzigo huo.

Gacaca iyatizame malalamiko yake aliyoyatoa mahakamani kwa umakini kuwa, baada ya kesi kuanza kusikilizwa yeye akiwa shahidi wa upande wa mashitaka alikuwa akitishwa ili atoe ushahidi unaoegemea upande wa Serikali kwa lengo la kuwakandamiza washtakiwa hata kufikia hatua ya kuomba mahakama imlinde dhidi ya ushahidi atakaoutoa.

Mahakama ya Gacaca irejee mwenendo wa kesi na hukumu mbalimbali ambazo mashahidi walipata kuiomba mahakama iliwalinde dhidi ya ushahidi wao, msingi wa maombo hayo ulikuwa nini na baada ya kutolewa kwa ushahidi, tuzo ya ushindi uliangukia upande upi?

Gacaca iwasikilize wazee wa baraza ambao ni wachokonozi. Isikilize hoja yao kwamba mara nyingi shahidi anapoomba mahakama imlinde dhidi ya ushahidi ataoutoa anakuwa amepigwa msasa mahali.Nna kama wachokonozi wana maelezo ya maandishi yanayoiomba Gacaca imtake shahidi atoe maelezo ya kina na ushahidi usiotia shaka wa madai yake kuwa kuna watu walikuwa wakimtisha na kumtesa ili atoe ushahidi wanaoutaka wao, mahakama itoe amri kwa shahidi huyo kuwasilisha ushahidi wa madai yake unaowataja wahusika wa vitisho hivyo.

Gacaca imlazimishe shahidi huyo aseme makachero au hao waliokuwa wakimtesa kwa sharti la kumtaka ieleze mahakama kile wanachotaka wao, walitumwa na nani? na kipi hicho alichokuwa akilazimishwa aseme?Kisha imtake arudie kutoa ushahidi wake upya bila kumuhofia binadamu isipokuwa Mungu na hii ni kwa sababu sasa hawezi kushtakiwa tena kwani ana ulinzi wa mahakama dhidi ya ushahidi wake wa awali. Baada ya hapo Gacaca ifunge faili la shahidi huyu kisha ifungue faili la Muna.

Bila kujali kama Muna atakuwepo Gacaca au lah! ipokee maombi ya wachokonozi ya kupitiwa upya; kwanza kwa mwenendo wa maisha ya Muna uraiani baada ya mumewe mpenzi, Mohamedi Hariri kutupwa gerezani.

Gacaca ipokee madai yanayohusu Muna kuwa na uhusiano binafsi nje ya aliokuwa nao baada ya mumewe kutupwa gerezani na ikubali kufanyika kwa uchunguzi wa kienyeji utakaothibitisha hilo ili kumsafisha na tetesi zinazozidi kuzagaa uchokonozini kila uchao.

Uchunguzi ulenge kujua alihusiana na nani? historia ya huyo aliyekuwa akihusiana naye ikoje? alikuwa akikutana naye wapi na alikuwa akifanya jitihada zozote za kumnasua mumewe Hariri kutoka gerezani au lah na nani alikuwa akimsaidia?

Pamoja na mambo mengine mengi ambayo Gacaca itaona yanafaa kutizamwa kwa macho matatu, iangalie Muna, mwanamke mrembo na aliyejipatia umaarufu mkubwa gerezani kutokana na kutembelewa mara kwa mara na mtu mwenye ukwasi mkubwa alikuwa akijishughulisha na nini baada ya mumewe Hariri kukamatwa na kama yupo aliyekuwa akimsaidia kiuchumi ni nani?

Kisha Gacaca ifanye marejeo ya maisha ya Muna gerezani. alikuwa akiishi maisha ya aina gani ukiachilia mbali ucha mungu wake.

Ieleweke hapa kuwa mtu anapopelekwa gerezani hupewa namba ambayo hutumika kama akaunti yake hivyo anapoletewa fedha na ndugu, jamaa au mpenzi wake huwekewa katika akaunti yake hiyo.

Anapohitaji kitu mfungwa au mahabusu hufika ofisi za gereza na mhasibu huorodhesha mahitaji yake kwa ajili ya kwenda kumnunulia katika duka la magereza kutoka kwenye fedha zilizo kwenye akaunti yake na yeye hufika kuvichukua.

Lakini pia wapo wafungwa au mahabusu ambao wana vijakazi gerezani kutokana na ukwasi mkubwa wanaokuwa nao. Hawa huwatumikia kama watumikavyo mayaya majumbani.

Sasa Gacaca iangalie, je! Muna alikuwa na ukwasi kiasi gani katika akaunti yake ya gerezani? kuna siku ukwasi huo uliwahi kushuka chini ya sh milioni moja? nani alikuwa akiijaza mamilioni akaunti ya Muna gerezani?

Hili litasaidia kuondoa minong’ono kuwa Muna alikuwa na mtu nyuma yake na litathibitisha; kama itathibitika kuwa kweli, kuwa Muna alikuwa akitumia fedha za jasho lake kisha Gacaca ilifunge faili lake.

Kwa sababu Gacaca ni mahakama ya kienyeji isiyofungwa na taratibu za vitabuni katika kuendesha mambo yake iahirishe usikilizwaji wa shauri hili mpaka itakapotangaza tarehe nyingine ndani ya siku saba ambapo mwelekeo wa iwapo kuna watu wengine wanapaswa kujumuishwa katika shauri hili utajulikana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here