NASMA MAYUNGA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeivua taji la ubora wa utoaji huduma Bandari ya Mombasa, Kenya na imezipiga mawimbi mazito Bandari za Cape Town na Durban za Afrika Kusini yaliyozitisa pembeni ya uringo wa ubora.
Heka heka na kupigana vikumbo usiku mchana kwa vigogo, maafisa na watumishi wa TPA wanaopambana kuboresha utoaji huduma kwa Bandari za Tanzania, hatimaye vimeiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kupanda viwango vya ubora wa utoaji huduma, ikizipiku Bandari za Mombasa, Durban na Cape Town.
Ifahamike kuwa kwenye ulimwengu wa usafirishaji wa majini kimataifa, ushindani haupimwi kwa maneno au siasa, bali ubora wa teknolojia unaorahisisha kasi ya upakuaji mizigo, ubora wa miundombinu ya bandari, usalama wa shehena inapokuwa bandarini na ufanisi wa utendaji kwa ujumla.
Tangu TPA ilipoanza kufanya maboresho ya bandari zake, vita baridi ya nani anashikilia usukani wa ubora wa utoaji huduma kwa bandari zilizo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi zinazolisha mataifa yasiyo na pwani ya Afrika Mashariki na Kusini; imekuwa ikipiganwa kwa kificho na waziwazi.
Lakini hatimaye majibu yametoka na kengele ya ushindi imelia katika viunga vya TPA, ambako kumepokelewa ripoti mpya ya Benki ya Dunia inayoonyesha viwango vya ubora vya utoaji huduma kwa bandari zote duniani iliyoipa Bandari ya Dar es Salaam nafasi ya 255.
Kwa jicho la haraka, mtu anaweza asielewe uzito wa namba hii. Lakini kwa wafanyabiashara, wachumi na magwiji wa usafirishaji huu ni mtetemeko wa ardhi.

Bandari ya Cape Town, Afrika Kusini.

Namba hii inamaanisha jambo moja kubwa. Kuwa, Bandari ya Dar es Salaam imeivua taji Bandari ya Mombasa (Kenya) na kuziacha hoi Bandari za Durban na Cape Town (Afrika Kusini). Dar es Salaam sasa ndiyo lango kuu la usafirishaji wa majini la uhakika na la kibabe zaidi katika ukanda huu.

Bandari ya Mombasa, Kenya.

Kupata ushindi huu dhidi ya miamba ya muda mrefu ya usafirishaji wa majini haikuwa bahati mbaya. Ilihitaji akili nyingi, uwekezaji mkubwa na maamuzi magumu.
Na ili kujua mbinu zilizotumika kuleta ushindi huu wa kihistoria ambao umeleta fahari kwa watanzania wote, Tanzania PANORAMA imekutana na kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Abed.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Aned.
Katika mahojiano haya, Mkurugenzi Abed anaeleza siri za kufikiwa kwa mafakanikio hayo kuwa ni uboreshaji wa mifumo ya kidijitali, ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa na uboreshaji wa bandari.
Macho sasa kwenye kilele baada ya kuzitawala Bandari za Afrika Mashariki na Kusini. Je, Bandari ya Dar es Salaam ina mkakati gani mpya wa kuvunja rekodi na kuingia kwenye orodha ya bandari bora zaidi duniani?
Vuta kiti chako keti kitako, weka kahawa yako pembeni ufuatilie mahojiano haya ambayo yatabaki kuwa rejea muhimu ya safari ngumu ya mafanikio ya Bandari za Tanzania kwa miaka elfu lela ulela.
Hii siyo tu stori ya bandari. Hii ni stori ya furaha kwa watanzania kushinda vita vya kiuchumi vinavyopiganwa sasa duniani kote.
Mkurugenzi Abed anaanza kwa kueleza kuwa Bandari ya Dar es Salaam, imepanda hadi nafasi ya 255 duniani katika ripoti ya ufanisi wa bandari za makontena (Container Port Performance Index – CPPI), ikitoka nafasi ya 360 iliyokuwa awali jambo linaloashiria kuongezeka kwa ufanisi kiutendaji.
Maboresho na mambo yaliyochangia Bandari ya Dar es Salaam kuwa kinara kwa Bandari za Afrika Mashariki na Kusini, ikiziacha nyuma Bandari ya Mombasa ambayo ipo nafasi ya 396, Durban (Afrika Kusini) nafasi ya 398 na Cape Town (Afrika Kusini) nafasi ya 400 ni haya yafuatayo.

Bandari ya Durban, Afrika Kusini.

Mosi ni kupungua kwa muda wa meli kusubiri bandarini; maboresho makubwa na yaliyotumia gharama kubwa yaliyofanywa na TPA katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo yamepunguza muda wa meli za makontena kukaa au kusubiri kuhudumiwa.
Kwamba, awali muda wa meli za makontena kusubiri kuhudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam ulikuwa siku 10 hadi 12 lakini hivi sasa baada ya maboresho yaliyofanyika, muda wa kusubiri ni siku moja hadi tatu tu.
Kwa maneno yake mwenyewe, Mkurugenzi Abed anasema; “Ukienda kwenye utendaji wa meli moja hadi nyingine kwa upande wa meli za makasha ambazo zinahudumiwa katika bandari yetu ya Dar es Salaam, hapo awali muda wa kusubiri meli zikiwa nangani ilikuwa zinachukua siku zaidi ya 30.
“Lakini kwa sasa meli za makasha, tunasema zina base on arrival yaani zikishafika zinafunga moja kwa moja. Lakini vile vile muda wa meli kuhudumiwa ikiwa gatini mwanzoni tulikuwa tunachukua kati ya siku 10 hadi 12 kuhudumia meli yenye makasha 3,000 lakini kwa sasa meli yenye makasha 3,000 inahudumiwa ndani ya siku moja na nusu hadi mbili ikizidi sana siku tatu.
“Na hivi vyote ndiyo vipimo ambavyo wenzetu wa Benki ya Dunia wanavitumia kupima ubora wa utoaji huduma.”
Mkurugenzi Abed anataja pia uwekezaji kwenye miundombinu kwa kueleza kuwa; “Serikali na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamewekeza katika ununuzi wa vifaa vya kisasa na ujenzi wa magati na miundombinu ya kuhifadhi shehena.
“Haya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha hapa ilipo sasa Bandari ya Dar es salaam.

Bandari ya Dar es Salaam.

“Ujenzi wa miundombinu. Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na mradi mkubwa wa uongezaji wa kina cha maji.
“Unapoongolea ukubwa wa bandari lazima iweze kupokea meli kubwa. Kwa hiyo tumeongeza kina cha maji kutoka mita 11.7 hadi kufika mita 14.5 katika magati yetu. Hii sasa inaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kupokea meli zenye kina cha mita 13.5 na urefu wa mita 305.
“Kwa hiyo ongezeko hili la uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam limechagiza ongezeko la shehena katika bandari hii.
“Lakini si hivyo tu, katika Bandari ya Dar es Salaam kumefanywa maboresho makubwa kwenye vitendea kazi; kwa maana vitendea kazi kwa ajili ya kupakua shehena za makontena, lakini vile vile mizigo mchanganyiko na mizigo ya kichere.
“Kwa hiyo haya yote kwa ujumla yameleta matokeo chanya sana katika bandari hii ya Dar es Salaam. Isitoshe tu kuwa na vifaa vya kutosha, unaweza kuwa na miundobinu ya kutosha lakini ukakosa ujuzi na teknolojia ya kutosha katika kuhudumia shehena. Ujuzi na teknolojia katika Bandari ya Dar es Salaam sasa vipo juu sana.”
Kisha Mkurugenzi Abed anageukia ushirikiano na waendeshaji binafsi kwa kueleza kuwa ubia na ushirikiano wa kimkakati na waendeshaji wa kimataifa kama Kampuni ya DP World umeongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo.
“Kwa hiyo, mwaka 2024 serikali ilifanya uamuzi sahihi sana kuleta waendeshaji binafsi ambapo sasa hivi Bandari ya Dar es Salaam tuna waendeshaji binafsi wawili; kwa maana ya DP World ambaye anaendesha gati namba sufuri mpaka gati namba saba.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya DP World Tanzania, Martin Jacob.
“Mwingine ni Tanzania East Africa Gateway Terminal ambaye anaendesha gati namba nane mpaka gati namba 11.
“Kwa ujumla miundobinu bora, teknolojia bora ya vitendea kazi lakini vile vile ujuzi bora wa waendeshaji binafsi umesababisha utendaji wa bandari yetu kukua kwa kiasi kikubwa.
“Kwa hiyo baada ya haya yote kuungana kwa sasa tuna uzoefu wa usanifu wa hali ya juu katika bandari yetu ya Dar es Salaam. Kama tulivyosema kwamba huu ushirikishwaji umeongeza pia network ya wateja.
“Wateja wengi sasa wana imani na Bandari ya Dar es Salaam. Hivi karibuni tumeenda kwenye rekodi mpya ya kuhudumia zaidi ya makasha 21 ndani ya masaa 24. Na hii imetokana na utendaji bora wa waendeshaji wetu ambao wanafanya kazi katika bandari hii.
“Kutokana na utendaji bora ndio maana tunaona bandari hii inaendelea kuwa kinara katika uhudumiaji wa shehena hasa shehena ya makasha.
“Nikitaka kutoa taarifa tu kuhusiana na utendaji wetu ndani ya miaka miwili iliyopita kabla hatujaungana na waendeshaji binafsi; mwaka 2023/24 tulihudumia tani milioni 23.7 lakini mwaka mmoja baadaye baada ya kuhusisha waendeshaji binafsi na kufanya maboresho mengine ya vitendea kazi, mwaka 2025/2026 tuhudumia tani milioni 33.7.
“Hii inamaanisha ndani ya miaka miwili ambayo tumefanya maboresho ya vitendea kazi, vile vile ushirikiano na waendeshaji binafsi tumeweka tofauti ya tani milioni 10 jambo ambalo halijawahi kutokea hapo awali.”
Mkurugenzi Abed anazungumzia pia kuimarika kwa usafirishaji wa mizigo kwenda nchi za jirani za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi na Malawi kuwa kumepunguza mkwamo wa mizigo.
Kwamba kwa kutambua kwamba nchi zinazozunguka Tanzania zina mchango mkubwa kwa Bandari ya Dar es Salaam kufikia viwango vya juu kimataifa, TPA ilitengeneza mipango madhubuti iliyosaidia mizigo ya nchi hizo kufika kwa wakati na usalama wa hali ya juu.
“Tuna ofisi Rwanda, Burundi na Malawi; huko kote tumeweka ofisi kwa ajili ya kupokea maoni na mawazo ya wateja, lakini vile vile kuwarahisishia wateja biashara zao pale wanapotaka kutumia Bandari ya Dar es Salaam.
“Kazi nyingine ya ofisi hizi ni kushawishi wateja wapya kutumia Bandari ya Dar es Salaam na wateja waliopo kuendelea kupata huduma yetu.
“Pia tuna ushirikiano mzuri na jirani zetu; kwa mfano hivi karibuni rais wetu alikwenda kuzindua meli nne eneo la Ziwa Tanganyika ambazo zitashiriki kusafirisha mizigo kutoka Congo kuja Tanzania, hasa madini ambayo yanachimbwa upande ule.
“Lakini katika juhudi za kuwezesha utendaji kazi wa meli hizo, sisi tayari tumeshajenga Bandari ya Karema ambayo ina uwezo mkubwa wa kupokea shehena.

Bandari ya Karema

“Tunaendelea kuboresha Bandari ya Kigoma ambayo nayo itakuwa inachukua shehena hizo.”
Hapo anaweka tuo kidogo kisha anaendelea kuzungumza;
“Katika Bandari ya Dar es Salaam zimenunuliwa mashine za kisasa kabisa. Kwa mfano upande wa DP World kuna mashine zinaitwa Ship-to-Shore Gantry Cranes, ziko tano ambazo ni za kisasa zaidi.
“Halafu kuna mashine zingine za upande wa yadi, tunaita RTG zimenunuliwa hivi karibuni, zipo nane. Wakati DP World inakuja ilileta nane sasa na hizi mpya jumla zinakuwa 16 mpya za kisasa kabisa ambazo zipo katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Kuwepo kwa mashine hizi kumeongeza kasi ya uhudumiaji wa shehena. Kama nilivyosema awali kuwa zamani meli yenye wastani wa kontena 3,000 ilihudumiwa kati ya siku 10 hadi 12 lakini hivi sasa ni ndani ya siku tatu tu.
“Na nilikuwa sijawaambia tu. Tunatarajia kujenga gati zaidi mpaka zifike gati 22 kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Sasa, kwa uwekezaji huo, tunatarajia mpaka kufika mwaka 2031, Bandari ya Dar es Salaam itakuwa inahudumia tani milioni 62 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Plasduce Mbossa.
Kazi yangu mimi ni kusimamia kikamilifu oparesheni za Bandari ya Dar es Salaam. Ninaifanya kazi hiyo kwa bidii. Na hapa sasa nimpongeze Bosi wangu, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mkeli Mbossa kwa jinsi anavyojitoa kwa hali na mali kuhakikisha TPA inaendelea kuwa muhimili wa Taifa kiuchumi.
“TPA imefika hapa kwa kazi ya mikono yake na akili yake kubwa. Na huwezi kuzungumzia mafanikio ya Bandari za Tanzania ya sasa pasipo kumtaja kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan. Kwangu mimi itoshe kusema kuwa ana kheri Rais Mama Samia Suluhu Hassan.”
