RIPOTA PANORAMA
Musa Nasoro Kuji ameondoka kwenye utumishi wa umma akiacha alama ambazo hazitafutika kirahisi kwa miongo mingi katika sekta ya utalii na uhifadhi hapa nchini.
Kuji alianza safari yake ya utumishi wa umma kama mtumishi wa kawaida katika Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) hadi mapema 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alipomteua kuwa Kamishna wa Uhifadhi (CC) wa shirika hilo, nafasi aliyodumu nayo hadi Julai, 2026 alipohitimisha kipindi chake cha utumishi katika sekta ya umma.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Angella Kairuki akimvisha cheo cha Kamishna wa Uhifadhi (CC) wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Mussa Nasoro Kuji mwaka 2024
CC Kuji ameondoka TANAPA akiliacha likiwa kwenye kilele cha mafanikio ya ukusanyaji mapato, kuvutia watalii wa ndani na nje kutembelea hifadhi, kuitambulisha Tanzania kimataifa, kutekeleza kikamilifu malengo ya serikali na kutafasili kwa usahihi azma na ndoto za Rais Samia kuhusu kukuza utalii na uhifadhi nchini.
Alama za CC Kuji zinaonekana kuanzia Aprili 22, 2021 Rais Samia alipotangaza azma yake ya kukuza sekta ya utalii alipokuwa akieleza Dira na Mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita mbele ya Bunge, jijini Dodoma.
Rais Samia alisema kuwa katika awamu yake ya kwanza ya uongozi, licha ya kuwepo kwa janga la Corona, serikali yake itaendeleza mafanikio yaliyofikiwa na serikali ya awamu ya tano.
Alisema azma yake ni kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025 na mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 zilizokuwa zikikusanywa wakati huo hadi Dola za Marekani bilioni sita, mwaka 2025.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alisema hatua zitakazochukuliwa ili azma hiyo itimie ni pamoja na kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ikiwemo kukuza utalii wa mikutano, malikale na fukwe pia kuhamasisha wawekezaji kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo hoteli ili kupunguza gharama za malazi.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia Bunge.
Alipoingia ofisini mapema 2024, CC Kuji alianza kazi kwa kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa maliasili sambamba na kutatua changamoto za mipaka kati ya Hifadhi za Taifa na vijiji vilivyo jirani na mipaka ya hifadhi.
Katika mahojiano aliyofanya na Tanzania PANORAMA alipokuwa akitimiza mwaka mmoja ofisini, CC Kuji alisema alianza kazi kwa kuelekeza nguvu kubwa kwenye kuboresha maeneo ya malisho ya wanyamapori, kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu wanaoingia kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi na mkazo mkubwa ulikuwa kuzingatia maelekezo ya wizara,
“Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja 2023/2024 shirika liliibua na kuendekeza mazao mbalimbali ya utalii. Tumeshughulika kwa nguvu kubwa na miundombinu korofi ndani ya hifadhi zetu na tulikabiliana na athari za mvua za Elninyo zilizotikisa dunia na kufanikiwa kuzuia athari hasi kwa biashara ya utalii nchini.
“Lakini pia, mimi na wenzangu kwenye menejimenti tulijifunga kibwebwe kuimarisha mazingira ya utendaji kazi na tumeshirikiana kikamilifu na wadau wa utalii kuandaa maonesho na matukio mbalimbali yanayohusiana na sekta ya utalii.
“Hayo yametuwezesha TANAPA kwa mwaka huu mmoja niliokaa ofisini kama kiongozi mkuu wa shirika hili kuongeza idadi ya watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa kwa asilimia 11 na kiasi cha mapato yaliyokusanywa yamevuka lengo kwa asilimia 21.” Maneno ya CC Kuji alipofanya mahojiano na Tanzania PANORAMA, mwaka 2024.
Taarifa rasmi ya TANAPA ya mwaka 2023/2024 ambayo Tanzania PANORAMA iliiona ilionyesha kuwa kati ya julai mosi, 2023 hadi juni 30, 2024 watalii 1,863,108 walitembelea Hifadhi za Taifa, ikiwa ni watalii 33,028 zaidi ya lengo lililowekwa na serikali la watalii 1,830,080.
Na kwa upande wa mapato, taarifa ilionyesha kuwa katika kipindi hicho, shirika lilitarajia kukusanya mapato ya Shilingi 382,307,977,497 lakini makusanyo yalifikia Shilingi 410,902,998,132.31 ambayo yalikuwa na ziada ya Shilingi bilioni 25.5.
CC Kuji aliendelea na mwenendo huo wa mafanikio kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo alisimamia kukamilifu utekelezaji wa ahadi ya serikali kwa watanzania.
Ahadi hiyo ambayo ilitolewa na Rais Samia ipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 iliyokasimiwa kiutekelezaji kwa TANAPA na ilitekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana akisoma hutoba ya bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2024/2025 iliyosomwa bungeni na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Angellah Kairuki ilieleza kuwa TANapa lilikuwa la kwanza miongoni mwa mashirika mengi ya serikali kumaliza mwaka huo wa bajeti likiwa limevuka malengo ya utekelezaji wake kwa zaidi ya asilimia 100.
Kwamba mwaka 2024/2025 ulikuwa mwaka wa kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia ya kuimarisha sekta ya utalii kwa kuifanya kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa sambamba na kutoa fursa kwa watanzania hususan vijana kushiriki kujenga uchumi wa taifa lao kupitia sekta ya utalii.
Ripoti nyingine ya mwenendo wa utekelezaji kazi za TANAPA kwa mwaka huo wa fedha ambayo Tanzania PANORAMA ilipata kuiona, inaonyesha kuwa CC Kuji alifanikiwa sana baada ya kuweka nguvu kubwa kwenye kuimarisha miundombinu ya utalii, doria za kukabiliana na ujangili na matumizi ya teknolojia ya kisasa kuboresha ulinzi na usimamizi wa wanyamapori.

Uwanja wa ndege wa Soronera.
Inaonyesha zaidi kuwa CC Kuji na menejimenti yake walizingatia uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vilivyo jirani na hifadhi, kudhibiti mimea vamizi na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege ndani ya Hifadhi za Taifa.
Kwenye korido za ofisi za makao makuu ya TANAPA, CC Kuji alitazamwa na watumishi wenzake kwa jicho la muongoza njia na pia alipewa jina la utani la mwanafunzi bora wa mama kutokana na kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais Samia.
Hilo linaonekana kwenye utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kwa TANAPA ikiwemo kuanzishwa kwa mazao mapya ya utalii ambapo CC Kuji alisimamia kuanzishwa kwa utalii wa kuogolea kwenye chemchem ya maji moto katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, utalii wa kuruka kwa ndege ndogo katika Hifadhi za Taifa za Kilimanjaro, Arusha na Ziwa Manyara pamoja na utalii wa kulala nje kuangalia nyota katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Alama za CC Kuji alizoacha TANAPA zina mnyororo mrefu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa gofu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na jina la Afande Kuji linatajwa tena kwenye uanzishwaji wa utalii wa historia.

Kamishana wa Uhifadhi Mstaafu, Musa Kuji akisaliamiana na Chifu wa sita wa kabila la wahehe, Mtwa Abdul II Abdul Adam Sapi Mkwawa.
CC Kuji, akisimamia utekelezaji wa azma ya Rais Samia na malengo ya serikali, aliibua upya utalii wa historia hasa katika mikoa ya Iringa na Kigoma hivyo kutoa fursa kwa watanzania na watalii kutoka nje ya nchi kufanya utalii wa historia na kujifunza historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Vivutio adhimu vya utalii wa historia vilivyopewa kisogo kwa muda mrefu kabla ya kuibuliwa na CC Kuji akiwa Kamishna wa TANAPA ni pamoja na makumbusho ya Dk. David Livingstone iliyopo Ujiji, Kigoma.

Njia ya watumwa iliyopo Ujiji, Kigoma.
Katika makumbusho hiyo ya Dk. Livingstone imehifadhiwa historia ya kukutana kwake na Henry Stanley, Novemba 10, 1871. Wazungu hao wawili walikutana chini ya mwembe ambapo sasa pamejengwa mnara.
Stanley, mwandishi wa habari mmarekani alitumwa na mhariri wake kuizunguka Afrika nzima kumtafuta Dk. Livingstone akiwa hai au mfu ambaye habari zake zilitapakaa Ulaya na Marekani; Akaja kumkuta eneo la Ujiji, Mkoa wa Kigoma nchini Tanganyika.
Pamoja na vivutio vingine vingi vilivyoibuliwa na kuingizwa kwenye vitita vya utalii wakati wa uongozi wake, ipo pia njia ya watumwa na biashara ya meno ya tembo inayoanzia Ujiji, Kigoma hadi Bagamoyo, Pwani pamoja na Kanisa Katoliki la kihistoria la Ujiji, Kigoma.
Mkoani Iringa, CC Kuji alifika na kukutana na chifu wa sita wa kabila la wahehe, Mtwa Abdul II Abdul Adam Sapi Mkwawa ambako sasa wanazuoni na wanahistoria kutoka pande zote za dunia wamekuwa wakitembelea kujionea kaburi la Nyundo, mahali walikozikwa mamia ya wanajeshi wa kijerumani walioangamizwa na Chifu Mtwa Mkwawa wakati wa vita ya kwanza kati ya majeshi ya Chifu Mkwawa na wajerumani.
Pia kisima cha ajabu kinachojulikana kwa jina la Kikongoma alipopotelea mama mzazi wa Chifu Mkwawa mwaka 1889, Kaburi na Chifu Mkwawa, kitanda cha jiwe alicholala kwa miaka minne wakati akipambana na wajerumani na pango aliloishi wakati wote wa mapambano yake hayo kabla ya kujiua kwa kujipiga risasi kichwani.
Haina shaka hata kidogo kuwa hayo yote ndiyo yaliyomsukuma aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Hazara Chana, Novemba 14, 2024 kueleza hadharani kuwa anafurahishwa sana na kazi kubwa inayofanywa na TANAPA.

Rais Samia akipokea tuzo iliyotwaliwa na TANAPA kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu kijaji.
Lakini pia CC Kuji akiwa TANAPA alimfanya Rais Samia awe akinusa harafu ya marashi ya tuzo za kimataifa za utalii na uhifadhi kila wafanyakazi wa shirika hilo walipokuwa wakirejea nchini kutoka ughaibuni.
TANAPA ikiwa chini ya CC Kuji iliiwezesha Hifadhi ya Taifa Serengeti kunyakua tuzo ya hifadhi bora duniani kwa mwaka 2025 na tuzo ya kivutio cha wanyama wakubwa watano.
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ilinyakua tuzo ya hifadhi bora ya milima barani Afrika na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ilinyakua tuzo ya hifadhi bora kwa mandhari ya kuvutia.
Tuzo nyingine zilizonyakuliwa na TANAPA chini ya CC Kuji ni tuzo ya hifadhi bora kwa utalii iliyotwaliwa na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ilitwaa tuzo ya hifadhi bora kwa fungate.

Tuzo mbalimbali zilizonyakuliwa na TANAPA.
Historia itamkumbuka pia CC Kuji kwa kuiwezesha Tanzania kutangazwa kuwa nchi bora ya utalii wa safari duniani kwa mwaka 2025 na Zanzibar kutangazwa kuwa eneo bora la mikutano na matukio ya biashara pamoja na tuzo nyingine nyingi zilizohifadhi vema kwenye kabati la chuma la kuhifadhi tuzo za kimataifa lililopo TANAPA.
CC Kuji ameondoka kwenye utumishi wa umma Tanzania ikiwa imetembelewa na watalii 5,935,561 kwa mwaka 2025 ambalo ni ongezeko la asilimia 10.7 ikilinganishwa na watalii 5,360,247 waliotembelea Tanzania mwaka 2024.
Takwimu za mwenendo wa utalii nchini zilizosomwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji alipokuwa akiwasilisha hotuba ya wizara anayoiongoza kwenye Bunge la Bajeti mapema mwaka huu mjini Dodoma zinaonyesha kuwa hadi CC Kuji anaondoka ofisini, Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya tatu duniani kwa soko la utalii lililofanya vizuri mwaka 2025.
Haijapata kutokea kudhani likawa kosa. Hivyo kwa sababu kudhani haidhaniwi kuwa kosa; ni dhana ya makala haya kuwa watanzania hawamdai utumishi uliotukuka CC Kuji, aliyeondoka ofisini mapato ya utalii yakiwa yameongozeka kutoka Dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 4.4 mwaka 2025 ambalo ni ongezeko la asilimia 12.82.

Aliyekuwa Kamishna wa TANAPA, Mussa Nassoro Kuji.

