Waziri wa Serikali za Mitaa nchini Uganda, Balaam Barugahara, ameagiza kukamatwa kwa mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Naiku iliyopo Wilaya ya Mbale, baada ya ukaguzi kubaini tofauti kubwa kati ya idadi ya wanafunzi walioripotiwa na waliopatikana shuleni.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya waziri kufanya ziara katika shule hiyo na kubaini kuwa, licha ya shule kuripoti kuwa na wanafunzi 1,352 walioandikishwa, ni wanafunzi 705 pekee waliokutwa wakiwa shuleni wakati wa ukaguzi.
Tofauti hiyo imeibua tuhuma za uwezekano wa kuwasilishwa kwa takwimu zisizo sahihi, kwa lengo la kupata fedha zaidi za ruzuku ya elimu kutoka serikalini.
Serikali ya Uganda imekuwa ikiimarisha ukaguzi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika sekta ya elimu, hususan katika mpango wa elimu ya msingi bila malipo (UPE), ambapo baadhi ya shule zimekuwa zikikabiliwa na tuhuma za kuongeza idadi ya wanafunzi ili kunufaika na fedha za serikali.
Mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.

