Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Jijini Mwanza kwa kushirikiana na Jopo la Madaktari b
Bingwa kutoka Chuo cha Upasuaji nchini Hispania, kwa mara ya kwanza imefanikiwa kufanya upasuaji wa kuwatenganisha watoto waliozaliwa wakiwa wameungana.
Hatua hiyo inatajwa kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Akizungumzia mafanikio hayo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Novath Ngowi, amesema mafanikio hayo ni historia kwa hospitali hiyo na yanaonesha kuwa uwezo wa kutoa huduma za kisasa za upasuaji kwa watoto wenye changamoto kubwa za kiafya umeendelea kuimarika.
Dkt. Ngowi ameongeza kuwa ushirikiano kati ya madaktari wa Bugando na wataalamu kutoka Hispania umewezesha kufanikisha operesheni hiyo, sambamba na kuwajengea uwezo madaktari wa ndani katika kufanya upasuaji mgumu wa aina hiyo hapo baadaye.
Baadhi ya wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji huo wameeleza furaha na shukrani zao kwa timu ya madaktari bingwa wa Bugando na wale kutoka Hispania, wakisema walikuwa wamepoteza matumaini ya watoto wao kupona kabla ya kufanyika kwa operesheni hiyo iliyofanikiwa.
Wakati huo huo, Jopo la Madaktari Bingwa kutoka Hispania kwa kushirikiana na Madaktari wa Hospitali ya Bugando linaendelea na kambi maalum ya siku tano katika hospitali hiyo, likitarajia kufanya upasuaji wa magonjwa mbalimbali ya tumbo kwa watoto wasiopungua 40.
Lengo la kambi hiyo ni kuimarisha huduma za kibingwa kwa watoto pamoja na kuwajengea uwezo madaktari wa ndani ili waendelee kutoa huduma za kiwango cha juu hata baada ya wataalamu hao kutoka nje kukamilisha ziara yao
