Sunday, 23 August 2026

BANDARI YA DAR ES SALAAM KUHUDUMIA TANI MILIONI 33.7 MWISHO WA MWAKA WA FEDHA 2025/2026

Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam inatarajia kuhudumia jumla ya tani milioni 33.7 za shehena ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni ongezeko la tani milioni sita ikilinganishwa na tani milioni 27.7 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2024/2025. Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es […]

Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam inatarajia kuhudumia jumla ya tani milioni 33.7 za shehena ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni ongezeko la tani milioni sita ikilinganishwa na tani milioni 27.7 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2024/2025.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed G. Abed, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce M. Mbossa, wakati wa kikao na Wanakwaya wa Kwaya ya Walimu ya Jiji la Mwanza pamoja na viongozi wa Shirikisho la Walimu Nyamagana, waliofanya ziara ya mafunzo bandarini tarehe 26 Juni 2026.

Akizungumza katika kikao hicho, amesema ongezeko la shehena linatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, hatua zilizoongeza uwezo na ufanisi wa bandari hiyo.

Ameeleza kuwa awali lengo lilikuwa kuhudumia tani milioni 30 za shehena ifikapo mwaka 2030, lakini kutokana na maboresho yaliyofanyika, lengo hilo limefikiwa mapema katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, katika miezi 11 ya mwaka wa fedha 2025/2026 bandari hiyo tayari imehudumia tani milioni 30.8 za shehena. Inatarajiwa kuhudumia zaidi ya tani milioni 2.9 katika mwezi uliosalia, na hivyo kufikisha jumla ya tani milioni 33.7 kabla ya mwaka wa fedha kuhitimishwa.

Aidha, amesema kuwa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuonyesha ukuaji wa kasi katika miaka ya hivi karibuni ambapo Mwaka wa fedha 2023/2024 ilihudumia tani milioni 23.7 za shehena, huku mwaka 2024/2025 kiwango hicho kikiongezeka hadi tani milioni 27.7, sawa na ongezeko la tani milioni nne ndani ya mwaka mmoja.

Kwa upande wao, Wanakwaya wa Kwaya ya Walimu ya Jiji la Mwanza pamoja na viongozi wa Shirikisho la Walimu Nyamagana walisema ziara hiyo imewapa fursa ya kujionea maboresho yaliyofanyika bandarini na kupongeza juhudi za Serikali katika kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, hatua ambayo imeendelea kuimarisha biashara na uchumi wa taifa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *