Mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 imetolewa na kukabidhiwa kwa vikundi vya wajasiriamali 53 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikiwa ni fedha zilizotokana na asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo kwa kipindi cha Robo ya Tatu na Nne mwaka wa Fedha 2025/2026.
Baadhi ya wanufaika wakizungumza mara baada ya kupokea mikopo hiyo, wametoa wito kwa jamii kutohofia kujitokeza na kuchukua mikopo hiyo ambayo imezidi kuwa chachu ya maendeleo kwa wajasiriamali wengi wenye nia ya kujikwamua kiuchumi hapa nchini.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi mikopo kwa vikundi vya wanufaika hao amesema halmashauri zinapaswa kuweka utaratibu wa kutumia vikundi vilivyofanikiwa kuhamasisha ukopaji na kutoa elimu kwa wanufaika ili waweze kufikia malengo yaliyotarajiwa.
Rugwa ametoa wito kwa viongozi ngazi za Halmashauri katika mkoa huo kuendelea kutoa hamasa kwa makundi ya wenye ulemavu na vijana ambayo yameonekana kusuasua kujitokeza na kujisajili kwa ajili ya kuchukua mikopo hiyo kwa hofu ya hatua zitakazochukuliwa baada ya kushindwa kufanya marejesho.
Aidha, amewataka wataalam kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii kuchukua hatua kadhaa ili kuhakikisha wanaonufaika na mikopo hiyo wanafikia malengo waliyojiwekea ikiwemo kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara, kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanufaika pamoja na kufuatilia marejesho kwa wakati.
Mikopo hiyo imehusisha vikundi vya wanawake ambavyo vimepatiwa Shilingi milioni 281.2, vijana shilingi milioni 300.8 na wenye ulemavu shilingi milioni 26.8
