Wednesday, 7 October 2026

TANI 1,014 ZA DAWA ZA KULEVYA ZIMEKAMATWA NCHINI KUANZIA MWAKA 2020 – 2025

Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya, nchini Tanzania mamlaka inayoshughulika na udhibiti na mapambano dhidi ya dawa hizo (DCEA) imetangaza mikakati kadhaa ikiwamo inayolenga kupunguza madhara ya kiafya, kijamii na kiuchumi kwa watumiaji na waraibu wa dawa za kulevya. Maadhimisho ya mwaka huu yaliyobeba kaulimbiu isemayo, “Ubunifu wa kimkakati: […]

Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya, nchini Tanzania mamlaka inayoshughulika na udhibiti na mapambano dhidi ya dawa hizo (DCEA) imetangaza mikakati kadhaa ikiwamo inayolenga kupunguza madhara ya kiafya, kijamii na kiuchumi kwa watumiaji na waraibu wa dawa za kulevya.

Maadhimisho ya mwaka huu yaliyobeba kaulimbiu isemayo, “Ubunifu wa kimkakati: Suluhisho la changamoto ya dawa za kulevya” kikanda yamefanyika Kisesa Wilayani Magu Mkoani Mwanza, huku baadhi ya watu waliowahi kuwa waraibu wa dawa hizo na baadaye kupona wakitoa shuhuda kuhusiana na athari za dawa za kulevya.

Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Ziwa, Wambura Msafiri akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ameitaja mikakati inayotekelezwa na DCEA kuanzia mwaka 2023 kuwa ni pamoja na kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya, kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya, kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya na kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ng’wilabuzu Ludigija amesema katika kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, DCEA katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 – 2025, imekamata tani 1,014 za dawa za kulevya za aina mbalimbali.

Juni 26 kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupiga vita dawa za kulevya, ambapo kwa kutambua umuhimu wa siku hiyo wananchi hualikwa na kuungana katika kutafuta suluhisho la pamoja la changamoto ya dawa za kulevya ambazo zinaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa, jamii na hata familia.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *