Sunday, 11 October 2026

BANDARI YA TANGA YATAJWA KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI NCHINI

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayubu Sebabili, amesema uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Bandari ya Tanga umeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kupanua shughuli za biashara na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi. Akifungua Maonesho ya 13 ya Biashara na Utalii ya Mkoa wa Tanga yanayofanyika katika Viwanja vya Mwahako jijini […]

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayubu Sebabili, amesema uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Bandari ya Tanga umeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kupanua shughuli za biashara na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.

Akifungua Maonesho ya 13 ya Biashara na Utalii ya Mkoa wa Tanga yanayofanyika katika Viwanja vya Mwahako jijini Tanga, Sebabili amesema ongezeko la magari kutoka nchi jirani zinazotumia bandari hiyo ni ushahidi wa mafanikio ya uwekezaji huo jambo linaloonesha kuongezeka kwa shughuli za biashara za kikanda kupitia bandari hiyo.

“Nimekuwa nikikutana na magari ya nchi jirani za Rwanda, Burundi, Zambia, DRC, Uganda na Malawi yanatoka na kuingia bandarini. Hii inadhihirisha kuwa uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga umepanua wigo wa kibiashara katika huduma za kibandari,” alisema Sebabili.

Awali, Afisa Mkuu wa Uhusiano wa Bandari ya Tanga, Peter Milanzi, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari hiyo, Salehe Mbega, amesema maboresho yaliyofanyika yamefungua fursa nyingi za biashara kwa Mkoa wa Tanga, na mikoa mingine nchini pamoja na nchi jirani.

Milanzi ameongeza kuwa uwekezaji huo umeongeza imani kwa watumiaji wa bandari hiyo, ambapo nchi zilizokuwa hazitumii Bandari ya Tanga sasa zimeanza kuitumia kutokana na kuimarika kwa miundombinu na huduma zake hata sasa Zimbabwe ni miongoni mwa nchi zinazotumia Bandari ya Tanga kwa shughuli zake za usafirishaji wa mizigo.

Katika maonesho hayo, Bandari ya Tanga inatumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za kibandari, tozo mbalimbali pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zinazopatikana bandarini.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ni, “Kuonyesha Sekta ya Kimkakati ya Mabadiliko ya Kiuchumi Kuunga Mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *