WATU wanne wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa kufuatia ajali ya basi la abiria la kampuni ya Mwasote iliyotokea Mei 31, 2026 katika eneo la Maji Mazuri, kando ya barabara ya Mbeya–Chunya mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 9:10 alasiri baada ya basi lenye namba za usajili T134 DFB aina ya Mitsubishi, lililokuwa likitoka Mbeya kuelekea Chunya, kuacha njia na kupinduka.
Amesema watu waliofariki ni wanaume watatu na mwanamke mmoja wenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 35 na 40. Miongoni mwa waliotambuliwa ni Hamza (30) na Matrida Mwabanganya mwenye umri wa kati ya miaka 30 na 36.
Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, watu 29 wamejeruhiwa wanaume 24 na wanawake watano na kwamba kati yao 11 waliendelea kulazwa kwa matibabu huku wengine 18 wakitibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva, Nehemia Sanga (50), mkazi wa Uyole, aliyeshindwa kulimudu gari katika eneo lenye kona kali na kusababisha kuacha njia na kupinduka,”amesema Kamanda Kuzaga
Ameongeza kuwa dereva huyo anaendelea kupatiwa matibabu chini ya ulinzi wa polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
