Bunge la Ghana limepitisha muswada mpya unaoharamisha mapenzi ya jinsia moja pamoja na shughuli zinazohusishwa na jamii ya LGBTQ+, hatua ambayo imezua mjadala mkali ndani na nje ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa muswada huo, mtu anayejitambulisha kama mpenzi wa jinsia moja, mtu aliyebadili jinsia au mwenye mahusiano ya jinsia zote mbili anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka mitatu gerezani. Aidha, sheria hiyo inapendekeza kuwepo kwa wajibu wa wananchi kuripoti vitendo vinavyokiuka masharti hayo kwa vyombo vya usalama.
Muswada huo bado unahitaji kutiwa saini na Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, ili kuwa sheria kamili. Tangu kuingia madarakani mwaka jana, viongozi wa kidini nchini humo wamekuwa wakimtaka kuimarisha sheria zinazopinga mahusiano ya jinsia moja.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameelezea wasiwasi wao kuhusu hatua hiyo. Human Rights Watch limesema sheria hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya watu wa LGBTQ+ na kuchochea mazingira ya kufuatiliana na kuripotiana miongoni mwa wananchi.
Mahusiano ya jinsia moja tayari yalikuwa yamepigwa marufuku nchini Ghana kupitia sheria zilizorithiwa tangu enzi za ukoloni wa Uingereza. Hata hivyo, waungaji mkono wa muswada huo wanasema unalenga kuimarisha zaidi sheria zilizopo na kulinda maadili ya familia pamoja na tamaduni za taifa.
Akiwasilisha muswada huo bungeni, John Ntim Fordjour amesema sheria hiyo inalenga kulinda familia na maadili ya kitamaduni ya Ghana. Aliongeza kuwa itafanya mfumo wa sheria uliopo kuwa mkali zaidi katika kushughulikia masuala yanayohusishwa na LGBTQ+.
Muswada huo pia unapendekeza adhabu kwa watu wanaojitambulisha kama washirika au wafuasi wa haki za LGBTQ+, jambo ambalo limeendelea kuzua mjadala mkali kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kujieleza nchini Ghana.
