Marekani imesema iko tayari kuanzisha upya mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa juhudi za kidiplomasia zitashindwa kuzaa matunda, huku mazungumzo kati ya pande hizo mbili yakiendelea kutafuta suluhu ya tofauti zilizopo.
Akizungumza leo Jumamosi mjini Singapore katika kongamano la kimataifa la viongozi wa ulinzi, wanajeshi na wanadiplomasia wa Asia, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alisema Marekani ina uwezo na utayari wa kuchukua hatua za kijeshi wakati wowote itakapohitajika.
“Uwezo wetu wa kuanza upya mashambulizi inapobidi upo, na tuko tayari sana,” alisema Hegseth, akiongeza kuwa hifadhi za silaha za Marekani zimeimarishwa kwa kiwango kikubwa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali duniani.
Kauli hiyo inakuja wakati wapatanishi kutoka Marekani na Iran wakiendelea na juhudi za kupunguza tofauti kubwa zinazokwamisha kufikiwa kwa makubaliano kuhusu masuala ya usalama na nyuklia.
Hegseth pia alisisitiza kuwa Marekani haijapunguza umakini wake katika eneo la Asia-Pasifiki licha ya changamoto za kiusalama zinazoendelea Mashariki ya Kati.
“Tunaweza kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja. Tunaongeza nguvu katika miundombinu yetu ya ulinzi na kuongeza uzalishaji wa silaha mara mbili, tatu hadi nne zaidi ili kuhakikisha mipango yetu yote ya operesheni inafadhiliwa na kutekelezwa ipasavyo duniani kote,” alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameelezwa kuwa bado anaamini katika suluhisho la kidiplomasia na anataka kufikiwa kwa “makubaliano makubwa” yatakayohakikisha Iran haipati uwezo wa kumiliki silaha za nyuklia.
Tamko hilo linaashiria kuendelea kwa msimamo mkali wa Marekani dhidi ya Iran, wakati jumuiya ya kimataifa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya mazungumzo yanayolenga kupunguza mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati.
