Saturday, 29 August 2026

WAZIRI MAVUNDE AWATAKA WAMILIKI WA LESENI ZA MADINI KINYWE KUANZA UCHIMBAJI MARA MOJA

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametoa wito kwa wamiliki wote wa leseni za uchimbaji wa madini kinywe nchini kuanza shughuli za uzalishaji mara moja kwa kuzingatia masharti ya leseni zao na Sheria ya Madini Sura ya 123, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa madini […]

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametoa wito kwa wamiliki wote wa leseni za uchimbaji wa madini kinywe nchini kuanza shughuli za uzalishaji mara moja kwa kuzingatia masharti ya leseni zao na Sheria ya Madini Sura ya 123, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa madini hayo duniani ifikapo mwaka 2030.

Mavunde ametoa kauli hiyo leo Mei 30, 2026 wilayani Ruangwa mkoani Lindi wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya ubia kati ya Serikali na kampuni za Grafica Resources pamoja na Eminent Minerals Limited, ambapo Serikali inamiliki asilimia 17 ya hisa na wawekezaji asilimia 83 kwa kila kampuni.

Katika hafla hiyo, Waziri Mavunde aliiagiza Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye Sekta ya Madini (GNT) kuanza mara moja mchakato wa mazungumzo na wamiliki wote wa leseni za uchimbaji wa madini kinywe nchini ili kukamilisha masuala ya ubia wa Serikali na kuhakikisha miradi hiyo inaanza uzalishaji kwa wakati.

Alisema Serikali tayari imechukua hatua dhidi ya kampuni ambazo hazijaanza shughuli za uzalishaji kwa mujibu wa masharti ya leseni zao kwa kuzitumia hati za makosa (Default Notice) kwa mujibu wa Sheria ya Madini.

“Ndiyo maana kampuni zote ambazo hazijaanza uzalishaji kwa mujibu wa masharti ya leseni zao tumeziandikia hati ya makosa. Kusaini kwetu mikataba leo hakutoi unafuu kwa wawekezaji hawa kutotekeleza uwekezaji wao kwa mujibu wa sheria ya madini,” alisema Mavunde.

Aidha, Waziri huyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa maelekezo na kuwezesha usimamizi madhubuti wa sekta ya madini, hatua ambayo imechangia kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji na ukuaji wa sekta hiyo.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa madini kinywe utaifanya Ruangwa na maeneo mengine yenye rasilimali hiyo kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani wa kimataifa pamoja na teknolojia ya kisasa inayotegemea madini hayo.

Waziri Mavunde pia amewataka wawekezaji kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania, hususan vijana wanaoishi katika maeneo yanayozunguka miradi hiyo, ili kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa jamii na kuchochea maendeleo ya maeneo husika.

Kwa sasa, Serikali inalenga kufanya mazungumzo na wamiliki wa leseni 27 za uchimbaji wa madini kinywe nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa madini hayo na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa Taifa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *