Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya vitendo vya kishirikina vinavyohusisha upigaji wa ramli chonganishi pamoja na kujichukulia sheria mkononi.
Akizungumza Mei 15, 2026 katika kijiji cha Ng’hesha Wilaya ya Itilima, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Chacha Maro amesema baadhi ya waganga wa tiba asili wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya upigaji wa ramli chonganishi vinavyoweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo mauaji, majeruhi na kusambaratika kwa familia.
ACP Maro amewataka wananchi pamoja na viongozi wa sungusungu kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola pale wanapohisi kuwepo kwa viashiria vya uhalifu.
Aidha, amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuvunja sheria za nchi kwa namna yoyote ile.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa ya Kanadi Lameck Lupiga amewahimiza wananchi kufuata taratibu za kisheria katika kutoa taarifa za uhalifu badala ya kutumia nguvu au kufanya maamuzi binafsi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’hesha, Bunga Nselema amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha amani na usalama katika kijiji hicho.





