LONDON, Uingereza
ARSENAL watakuwa Emirates kuwakaribisha Atletico Madrid, mchezo wa nusu fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaochezwa leo Mei 5, 2026.
Kesho, Bayern watakuwa nyumbani Allianz Arena kucheza na PSG, ikiwa ni nusu fainali nyingine ya marudiano baada ya ile iliyochezwa jijini Paris.
ARSENAL V ATLETICO
Arsenal ya kocha Mikel Arteta ilipata sare ya bao 1-1 ugenini nchini Hispania, hivyo safari hii Atletico Madrid wana kibarua kigumu cha kuhimili presha ya Emirates.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Atletico kucheza katika ardhi ya Uingereza msimu huu, ambapo ilipoteza mechi zote tatu zilizopita.
Septemba, 2025, iliifuata Liverpool pale Anfield na kufungwa mabao 3-2. Mwezi uliofuata, ilitua Emirates na kubamizwa mabao 4-0. Baadaye, ilivaana na Tottenham jijini London na kufungwa mabao 3-2.
Msimu huu, Washika Bunduki wa London hawajafungwa katika mechi zote 15 za Ligi ya Mabingwa walizocheza, wakati Atletico imechezea vichapo vitano.
BAYERN V PSG
Mechi ya nusu fainali ya kwanza ilishuhudia mabao tisa yakifungwa jijini Paris wakati PSG ilipopata ushindi wa mabao 5-4. Safari hii, watakuwa mjini Munich, Ujerumani.
Timu hizo zitakutana zikiwa zimetoka kujeruhiwa katika Ligi za ndani. PSG ilimazimishwa sare ya mabao 2-2, wakati Bayern nao walipata sare ya 3-3 dhidi ya Heidenheim.
Bayern wanategemea safu yao ya ushambuliaji yenye Michael Olise, Harry Kane na Luis Diaz, ambayo imeshafunga mabao zaidi ya 100 msimu huu.
Mabingwa watetezi, PSG, wataikosa huduma ya Achraf Hakimi lakini pengo lake katika eneo la beki wa kulia, Warren Zaire-Emery, ambaye atakuwa na kibarua cha kumdhibiti Diaz.
Tangu ilipobadilishwa jina kutoka Kombe la Ulaya na kuitwa Ligi ya Mabingwa, Madrid ndiyo timu pekee iliyowahi kuwa mabingwa mara mbili mfululizo.
Hivyo, matajiri wa Ligue 1, PSG, wanaisaka rekodi hiyo baada ya kubeba ‘ndoo’ ya mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, walipoifunga Inter Milan mabao 5-0 katika mchezo wa fainali.






