Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali inavitegemea kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari katika kulinda maadili ya Watanzania, kwa kuwa vinabeba jukumu la kuelimisha jamii kupitia taarifa sahihi na zenye maadili.
Amesema hayo Aprili 29, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmonyoko wa Maadili wa mwaka 2026/2027 hadi 2036/2037, akisisitiza kuwa bila ushirikiano wa wanahabari, maadili hayawezi kulindwa kikamilifu.
Makonda amesema vyombo vya habari ni daraja muhimu la kuelimisha jamii na kuzuia vitendo visivyofaa, akibainisha kuwa kama mambo mabaya hayataangaziwa na kukemewa, yataendelea kueneza.
Mkakati huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Septemba 24, 2024 mkoani Ruvuma, akielekeza kuundwa kwa mfumo wa kitaifa wa kushirikisha Serikali, familia na wadau wote katika kulinda maadili.
Kwaupande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmonyoko wa Maadili haujalenga wizara pekee, bali unawahusisha pia wananchi katika utekelezaji wake.
Dkt. Gwajima amesema kupitia mkakati huo, kazi ya kuratibu malezi na makuzi ya watoto pamoja na ustawi wa familia itakuwa rahisi zaidi na yenye matokeo chanya kwa jamii kwani mkakati huo utasaidia kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kujenga jamii yenye nidhamu, maadili mema na rasilimali watu bora kwa maendeleo endelevu.






