Klabu ya Paris Saint‑Germain ya Ufaransa imeipiga Bayern Munich ya Ujerumani 5-4 katika raundi ya kwanza ya mchezo wao wa Nusu Fainali, Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo miamba hao wa Ufaransa bado wana kibarua kigumu katika raundi ya pili ya mchezo wao ujao.
Kocha wa Paris Saint‑Germain Luis Enrique amesema timu yake italazimika kucheza kwa umakini mkubwa na kufunga mabao zaidi ugenini dhidi ya Bayern Munich wiki ijayo ili kuhakikisha inafuzu fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ameeleza kuwa mazingira ya ugenini Allianz Arena yanahitaji kiwango cha juu cha umakini na ubunifu wa kushambulia.
Mchezo huo wa kwanza umeingia kwenye historia kama nusu fainali yenye mabao mengi zaidi katika enzi ya sasa ya Ligi ya Mabingwa, ukionyesha ubora wa safu za ushambuliaji za timu zote mbili pamoja na changamoto katika safu zao za ulinzi.
Mashabiki na wachambuzi wa soka wameutaja mchezo huo kuwa moja ya mechi za nusu fainali zenye ushindani mkubwa na kusisimia kuwahi kutokea.






