March 5, 2026

EWURA YATANGAZA BEI YA PETROLI KUPAA

andilile

RIPOTA PANORAMA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo mpya za mwezi Machi, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk. James Andilile bei za bidhaa hizo katika soko la Ghuba ya Uarabuni zimeongezeka kwa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 9.8 kwa dizeli na asilimia 7.4 kwa mafuta ya taa kwa mwezi Machi.

Bei hiyo inaanza kutumika Machi 4, 2026, ambapo bei ya rejareja ya petroli jijini Dar es Salaam imeongezeka hadi Sh. 2,864 kwa lita kutoka Sh. 2,788 ya Februari, ikiwa ni ongezeko la Sh. 76. Dizeli imepanda kwa Sh. 157 hadi Sh. 2,858 kutoka Sh. 2,701, huku mafuta ya taa yakiongezeka kwa Sh. 186 hadi Sh. 2,932 kutoka Sh. 2,746.

Vilevile kwa Tanga, ambapo petroli sasa inauzwa Sh. 2,925 kwa lita kutoka Sh. 2,849, dizeli Sh. 2,919 kutoka Sh. 2,762 (ongezeko la Sh. 157) na mafuta ya taa Sh. 2,993 kutoka Sh. 2,807 (ongezeko la Sh. 186).

Mtwara petroli imeongezeka kwa Sh. 75 hadi Sh. 2,956 kutoka Sh. 2,881, dizeli imepanda kwa Sh. 157 hadi Sh. 2,951 kutoka Sh. 2,794 na mafuta ya taa yameongezeka kwa Sh. 187 hadi Sh. 3,025 kutoka Sh. 2,838.

Taarifa ya EWURA inaonyesha kuwa kwa ujumla dizeli na mafuta ya taa vimepanda kwa kiwango kikubwa zaidi ya petroli katika bandari zote tatu.

Aidha, gharama za uagizaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 0.07 kwa petroli, asilimia 10.76 kwa dizeli huku mafuta ya taa yakionyesha upungufu wa asilimia 5.41.

Hakukuwa na mabadiliko ya gharama za uagizaji katika bandari za Tanga na Mtwara.

Mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha pia yameongeza shinikizo, baada ya kiwango kinachotumika mwezi Machi kuongezeka kwa asilimia 8.54.

“Mamlaka inawaonya wauzaji wa rejareja na jumla kuzingatia kikamilifu bei kikomo zilizotangazwa, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka utaratibu wa bei,” imeeleza taarifa ya Mkurugenzi Andilile.