Monday, December 23, 2024
spot_img

WAINGEREZA WAKARIBISHWA KUWEKEZA NISHATI JADIDIFU

RIPOTA MAALUMU

KAMPUNI za Uingereza zimearikwa kuja nchini kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati husasn nishati jadidifu.

Ukaribisho huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza ulioongozwa na kiongozi wa timu ya ustawi endelevu, Euan Davidson, jijini Dodoma.

Mhandisi Mramba alisema lengo la Serikali ni kuingiza umeme mwingi kwenye gridi ya Taifa unaotokana na nishati jadidifu.

Alisema Tanzania ina uhitaji wa uwekezaji kwenye miradi ya nishati jadidifu ikiwemo umeme jua kwa ajili ya matumizi ya majumbani hasa kwenye sehemu zilizo nje ya Gridi ya Taifa na uwekezaji mkubwa wa umeme jua utakaoingia katika Gridi ya Taifa.

Mhandisi Mramba alisema tayari uwekezaji kwenye nishati ya umeme jua umeanza kupitia mradi wa Kishapu-Shinyanga (150MW) na uwekezaji mwingine utafanyika kwenye maeneo mengine nchini ikiwemo Mkoa wa Dodoma (200 MW).

Alizungumzia pia uwekezaji katika umeme unaotokana na upepo kuwa kuna maeneo tayari yametambuliwa ambayo yanaweza kuzalisha umeme huo ikiwemo Dodoma, Singida, Mbeya, Makambako, Same, Mara na Arusha ambayo yanahitaji ushirikiano katika uwekezaji.

“Tanzania tumebarikiwa vyanzo vingi vya nishati jadidifu kwani pia tuna hazina kubwa ya jotoardhi katika maeneo takriban 52 ambayo yakiendelezwa yatazalisha umeme kuliko Nchi ya Kenya ambayo sasa inazalisha umeme wa jotoardhi, takriban megawati 1000,” alisema Mhandisi Mramba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (Kushoto) akizungumza na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza ukiongozwa na kiongozi wa timu ya ustawi endelevu, Euan Davidson (wa kwanza Kulia) kuhusu maeneo ya ushirikiano katika Sekta ya Nishati, Septemba 25, 2024 jijini Dodoma.

Aidha, Mhandisi Mramba alieleza nia ya Tanzania kutumia nishati safi zaidi kuzalisha umeme ikiwemo nishati ya blue hydrogen inayotokana na rasilimali ya gesi asilia, bila kusahau matumizi ya nishati ya bayogesi hasa katika maeneo ya vijijini yenye mifugo mingi.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Mramba alisema Serikali inakusudia asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Alisema kusudio hilo ni utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unaoshirikisha Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi.

Mhandisi Mramba alizungumzia pia usambazaji umeme mijini na vijijini kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye eneo hilo.

Alisema asilimia 99 ya vijiji vina umeme na ifikapo Disemba mwaka huu, kila kijiji kitakuwa na huduma ya umeme.

Kiongozi wa timu ya ustawi endelevu kutoka Ubalozi wa Uingereza, Davidson alimshukuru Mhandisi Mramba kwa kutoa taarifa za kina za Wizara ya Nishati zitakazotumiwa na Uingereza kuangalia maeneo ya kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati.

Alisema mazungumzo yao yamekuwa na umuhimu kwani Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele na Uingereza katika masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji.

Mhandisi Mramba na timu hiyo pia walizungumzia kongamano la kimataifa la nishati litakalofanyika Tanzania mwaka 2025 ambapo Uingereza imeonesha nia ya kushiriki.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya