Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MWINYI AITAKA AFRIKA KUONGEZA KASI UKUAJI UCHUMI

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Afrika kwa pamoja kuanza safari ya kutekeleza mikakati iliyojadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu na kuwa na mtazamo wa pamoja katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa bara hilo na kuongeza tija ya vijana kupitia elimu bora na stadi za kazi.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere kuanzia Julai 25 na 26, 2023.

“Ni jukumu letu Waafrika kupitia kizazi hiki kupanga mstakabali wetu kwa kuhakikisha kwamba uwepo wa idadi kubwa ya vijana katika nchi zetu unakuwa na faida kwetu badala ya kuwa mzigo, kwa hakika mkutano huu umekuwa wa mafanikio kwa kuwa umetoa fursa muhimu ya kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu juu ya namna ya kutatua changamoto na kufikia malengo yaliyokusudiwa.”, amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Ameongeza kuwa, majadiliano hayo yametoa mwanga juu ya sera na uwekezaji unaotakiwa ili kutumia ipasavyo uwezo na idadi kubwa ya vijana ambao bara la Afrika inao. Aidha,  imekuwa kipimo tosha juu ya utayari wa Afrika kuwekeza katika elimu na mafunzo ya stadi za kazi ambavyo vinaweza kuongeza ajira na kuboresha tija kwa Afrika.

Aidha, amewashukuru Wakuu wa Nchi, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri na wajumbe wengine kwa kushiriki katika mkutano huo pamoja na michango yao yenye tija waliyoitoa ambayo imefanikisha mkutano huo na kusema kuwa mafanikio ya mkutano huo ni deni ambalo Tanzania inaweza kulilipa kwa kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa mkutano.

“Tunaahidi kuendeleza Azimio la Dar es Salaam kuhusu mtaji wa rasilimali watu katika bara la Afrika na nje ya bara hili, tunaishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wao, ni imani yetu kwamba Benki hii itaendeleza dhamira yake katika utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kupitia Azimio hilo juu ya mtaji wa rasilimali watu”, amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Katika mkutano huo, nchi zimebadilishana uzoefu wa njia na mbinu mbalimbali za kuharakisha kufikiwa kwa ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto ya rasilimali watu katika nchi za Afrika. Pia wamepata fursa ya kujadiliana kwa kina juu ya mikakati muhimu ya kufikiwa kwa elimu bora na afya kama nguzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya