JINA la Patricia Hillary halitasahaulika kwa urahisi katika muziki wa mahadhi ya mwambao wa Pwani unaofahamika zaidi kwa jina la taarabu asilia kutokana na sauti nyororo ya mwanamuziki huyo ambaye amedumu katika uimbaji kwa zaidi ya miaka 40 sasa.
Muziki wenye mahadhi ya mwambao wa Pwani ulianza kuvuma nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla miongo miwili hadi mitano iliyopita na baadhi ya majina yaliyovuma katika uimbai wa muziki huo ni la Patricia Hillary aliyetamba enzi hizo na wimbo wa njiwa pamoja na ule wa jamani mapenzi yananitatiza.
Historia ya mwanamuziki Patricia Hillary inaonyesha kuwa ni mwanajeshi mstaafu aliyedumu kwenye muziki wa taarabu asilia kwa zaidi ya miaka 40.
Kipaji chake cha uimbaji wa taarabu asilia kiliibuliwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) alipomaliza chuo na kuanza kuimba kanisani mkoani Tanga na mwaka 1980 wakati Jeshi likizunguka mikoani kutafuta vipaji, lilifika Mkoa wa Tanga na kuongea na mwenyekiti wa kijiji ambaye alikuwa baba yake mkubwa Patricia Hillary na pia kiongozi wa ngoma ya Mdumange ambayo ni ngoma maarufu sana mkoani humo.
Maafisa wa JWTZ walimwambia mwenyekiti huyo kuwa wanahitaji binti mwenye heshima, adabu na anayejielewa ambaye atakuwa mwajiriwa wa jeshi na mwenyekiti huyo mara moja alimchagua Patricia.
Katika mahojiano aliyoyafanya na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Patricia anaeleza kuwa baba yake alimwambia amechaguliwa kwenda kuwakilisha ngoma ya mdumange lakini hakuwa amewahi kuicheza ngoma hiyo zaidi ya kuimba kwaya kanisani.
“Walikaa kama siku tatu nikawa naelekezwa na baba yangu nitakavyoimba na baadaye walikubali wakasema huyu atatufaa mpaka kwenye taarabu,” anakaririwa akieleza Patricia.
Hapo ndipo safari yake kimuziki ilipoanzia. Alianza kwenye kituo cha mgambo Tanga ambako ilikuwa kambi yake ya kwanza na akiwa hapo alifanikiwa kuimba wimbo wake wa kwanza unaofahamika kama ‘mpenzi wangu wa jua,’ na baadaye alisafiri hadi Dar es Salaam ambako aliimba wimbo ya njiwa.
Katika mahojiano yake na BBC, Patricia Hillaty anaeleza kuwa alipochaguliwa kujiunga na jeshi mwaka 1980 lakini wazazi wake na Kanisa alikokuwa akiimba kwaya hawakumruhusu kirahisi kuondoka.
“Niliwaambia nahitaji kwenda kutafuta maisha nitarudi, wengi waliumia kwanini naondoka, walinishawishi sana nibaki lakini niliwaambia nakwenda kuiwakilisha Tanga, walisikitika lakini hawakuwa na namna.”
Patricia alikuwa mwanamke pekee aliyechaguliwa katika Wilaya ya Korogwe kujiunga na JWTZ wakati huo, wengi walikuwa wanaume lakini hivi sasa wana Korogwe huwa wanajipiga kifua kwa mafanikio yake na yeye mwenyewe aliieleza BBC kuwa wana Korogwe wanamshirikisha katika shughuli nyingi za harusi na burudani.
Sauti ya Patricia Hillary unaweza kusema ndio ile ya kumtoa nyoka pangoni. Katika miaka yake 40 ya uimbaji, sauti yake ipo vile vile, ya kuvutia na ina nguvu ile ile aliyoimba wimbo wa njiwa mwaka 1980.
“Naitunza sana sauti yangu, mimi nina vitu situmii kabisa kutokana na kuitunza hii sauti yangu maana ndio mtaji wangu na ndio ofisi yangu,” anakaririwa na BBC.
Patricia anasema hatumii kabisa maji baridi, vinywaji vikali ili kuitunza sauti yake lakini pia anafuata masharti kama vile kutokukaa muda mrefu bila kuimba. “Uimbaji pia una masharti na nayafuata, hutakiwi kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi.”
Patricia anakaririwa zaidi kuwa alijaaliwa kupata watoto wawili na mume wake ambaye ni marehemu kwa sasa na baadaye mtoto wake mmoja alifariki kwa ajali na kubaki na mtoto mmoja.
Anasema mbali na mtoto wake wa kumzaa ana kundi kubwa la vijana anaoishi nao kama watoto wake ambao ni watoto alioachiwa na wadogo zake na amewalea mwenyewe.
“Nilijaaliwa watoto wawili lakini nina watoto wengi nimeachiwa na wadogo zangu, nimewalea mwenyewe na ndio wamiliki wa kila kitu changu katika muziki.”
Anasema katika timu yake hiyo kuna wanamuziki, meneja na watayarishaji wa muziki pamoja na wasimamizi wa shughuli zote za kimuziki.
Akizungumzia mwanamuziki anayemvutia zaidi, Patricia anasema; ‘Nilikuwa napenda sana uimbaji wa Shakira Saidi, alikuwa ni muimbaji mzuri Afrika Mashariki.’
Anasema Shakira Saidi alimvutia zaidi kuingia katika taarabu na moja ya nyimbo zake alizokuwa akizipenda ni ‘akukatae hakwambii toka.’ “Alikuwa na nyimbo nyingi kama viva Frelimo, mapenzi ni kama donda, alinivutia kwa vitu vingi,” anasema.
Mwaka 2016 alistaafu jeshi na kuendelea na shughuli binafsi za uimbaji wa taarabu ambapo kwa sasa anajivunia kuimba katika hafla mbalimbali za Serikali anazopata mialiko, matamasha ya taarabu, harusi na hata katika majukwaa makubwa ya muziki kama Sauti za Busara