RIPOTA PANORAMA
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, jana alitoa hotuba katika mkutano wa tatu wa wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi; hotuba iliyobeba ujumbe mzito.
Hotuba hiyo aliitoa katika Ikulu ya Kremlin, iliyopo jijini Moscow, Urusi kabla ya kuhitimishwa kwa mkutano huo na ilibeba ujumbe mahususi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa viongozi wa Mataifa ya Afrika na Urusi, uliowasilishwa kwao na Dk. Mwigulu aliyemuwakilisha kwenye mkutano huo.
Alisema viongozi wa Afrika kwa umoja wao wanapaswa kuangalia mustakabali wa vijana wa Bara la Afrika, ambao wana uwezo mkubwa lakini wanakosa fursa kwenye soko la ajira.
“Muhimu kwetu sote kwa pamoja ni mustakabali wa vijana wetu kutokana na uwezo mkubwa walionao. Afrika inasimama kama bara changa zaidi duniani; hata hivyo, kila mwaka mamilioni ya vijana wa kike na wa kiume huingia kwenye soko la ajira kutafuta fursa ambazo hazipo.

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba .akiingia Ikulu ya Kremllin iliyopo Moscow, Urusi
“Ili kukabiliana na changamoto hii, ushirikiano wetu lazima ulenge kuwa na ubunifu wa hali ya juu.
“Ushirikiano katika masuala ya akili unde na teknolojia za kidijitali lazima uwe mahsusi ili tuweze kutoa mafunzo kwa kizazi kijacho cha wahandisi wa kiafrika, ambacho kitahakikisha kuwa data za kiafrika zinasalia chini ya udhibiti wa Afrika kwa kuzingatia mkakati wa umoja wa Afrika wa akili unde (African Union Continental AI Strategy),” alisema.
Alishukuru Shirikisho la Urusi kwa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kitanzania.
“Ili kuimarisha zaidi uendelezaji wa rasilimali watu, tunatamani kuongezewa mgao kwa kuzingatia zaidi nyanja muhimu za uhandisi, tiba na sayansi za hali ya juu,” alisema Mwigulu.
Katika hotuba yake hiyo, Waziri Mkuu Mwigulu aliwasilisha ombi maalumu kwa Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye wakubali Lugha ya Kiswahili iwe miongoni mwa lugha zinazotumiwa na jukwaa hilo ili kuimarisha uelewa miongoni mwa washiriki.
“Kiswahili siyo tu kwamba ni lugha rasmi ya kazi katika mikutano ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, UNESCO na taasisi nyingine kubwa za kimataifa, bali kwa miongo kadhaa imekuwa ikifundishwa kwa ufahari katika taasisi za kitaaluma za hapa Urusi.
“Ili kuimarisha uelewa wetu, Tanzania inapendekeza rasmi kwamba Kiswahili kijumuishwe katika mipango ya kitamaduni na kielimu ya Jukwaa la Ushirikiano wa Urusi na Afrika.

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nxhemba akishiriki mkutano wa tatu wa wakuu wa nchi na serikali za mataifa ya Afrika na Urusi katika Ikulu ya Kremlin, jijini Moscow, Urisi.
“Ninawapongeza Rais wa Mali na wenzake katika shirikisho hili walioamua kufanya mabadiliko ya kizalendo na kutumia lugha zao. Ninawaalika wabadilishe matumizi ya lugha za kikoloni na sasa watumie Kiswahili na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itawapatia walimu, vitabu vya kufundishia na kamusi.
“Huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kuileta Afrika nzima kuimiliki lugha hii badala ya kujivunia lugha hizo za kikoloni,” alisema Mwigulu.

WAkuu wa nchi na serikali za mataifa ya Afrika na Urusi wakiwa katika picha ya pamoja pembeni ya mkutano wao wa tatu uliofanyika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow Urusi.
Waziri Mkuu Mwigulu aliambatana na Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Frederick Kibuta, Makatibu Wakuu na watendaji wengine wa Serikali.
