Thursday, 20 August 2026

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO MKUU WA AFRICA50 NA JUKWAA LA MIUNDOMBINU AFRIKA

SCOLA MALINGA NA JOSEPH MAHUMI, WF-Dar es Salaam TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), utakaofanyika Agosti 5 na 6, 2026…

SCOLA MALINGA NA JOSEPH MAHUMI,

WF-Dar es Salaam

TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), utakaofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), kilichopo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alisema kaulimbiu ya mkutano huo ni miaka kumi ya mafanikio kutoka maono hadi utekelezaji na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan na pia mwenyekiti wa hafla ya ufunguzi wa mkutano.

Waziri Omar alisema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri na unatarajiwa kuvutia washiriki zaidi ya 1,200 kutoka ndani na nje ya Afrika, wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi za fedha za kimataifa, wawekezaji, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Alisema mkutano huo unafanyika kipindi muhimu ambapo Africa50 inatimiza miaka kumi tangu kuanza rasmi shughuli zake mwaka 2016. Africa50 ilianzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu barani Afrika.

“Tangu Tanzania imejiunga rasmi na Africa50, Februari 14, 2023 kama mwanahisa wa

kundi la nchi za Afrika (African Sovereign States) imepata fursa za kushiriki kikamilifu katika maandalizi, uendelezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya miundombinu” alisema Waziri Omar

Aidha, alitaja baadhi ya miradi ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi kwa ushirikiano na Africa50 kuwa ni pamoja na maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini Liquefied Natural Gas (Mini LNG), miradi ya miundombinu ya usafirishaji wa umeme, pamoja na upanuzi wa huduma za afya hususan matibabu ya kusafisha figo (dialysis) kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

Waziri Omar alisema shughuli zitakazotekelezwa siku mbili za mkutano huo ni mkutano mkuu wa wanahisa wa Africa50, jukwaa la miundombinu Afrika pamoja na hafla za kusaini makubaliano mbalimbali ya maandalizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu.

Alisisitiza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni fursa muhimu kujitangaza kimataifa kama kitovu cha uwekezaji wa miundombinu katika ukanda wa Afrika Mashariki, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha za kimataifa.

“Mkutano huu unatarajiwa kuchochea biashara, kuimarisha utalii wa mikutano (MICE), kuongeza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kuwapokea wageni watakaohudhuria mkutano huo muhimu wa kimataifa kwa kuwa unatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kimataifa yatakayofanyika nchini mwaka 2026 na unatoa jukwaa muhimu la kuendeleza ajenda ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *