Mashindano ya CECAFA Kagame Cup 2026 yamezidi kupata hamasa baada ya droo ya hatua ya makundi kukamilika na kuziweka timu mbalimbali katika makundi yenye ushindani mkubwa.
Mabingwa wa kombe la CRDB Tanzania, Simba SC, wamepangwa Kundi B pamoja na Singida Black Stars, Jamus FC ya Sudan Kusini na MCC ya Somalia.
Kundi hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkali, hasa kutokana na uwepo wa timu mbili kutoka Tanzania ambazo zinafahamiana vizuri na kila moja ikiwa na lengo la kuanza mashindano kwa matokeo mazuri.
Kundi A litakuwa na APR FC ya Rwanda, Vipers SC ya Uganda, Gor Mahia ya Kenya pamoja na Garde Républicaine ya Djibouti, huku Kundi C likiwa na Al Hilal ya Sudan, Rayon Sports ya Rwanda, Tusker FC ya Kenya na KVZ FC ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano, timu zitakazomaliza kileleni mwa makundi yao matatu zitafuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali. Nafasi moja iliyobaki itachukuliwa na timu yenye rekodi bora zaidi kati ya zile zitakazomaliza nafasi ya pili kwenye makundi.
Droo hiyo imeongeza hamasa kwa mashabiki wa soka Afrika Mashariki na Kati, huku Kundi B likitarajiwa kuwa miongoni mwa makundi yenye mvuto mkubwa kutokana na kukutana kwa Simba SC na Singida Black Stars.

