Rais wa Bassirou Diomaye Faye ametangaza serikali mpya ya Senegal yenye mawaziri 30, lakini hatua hiyo imeibua mvutano mpya wa kisiasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu na mshirika wake wa karibu, Ousmane Sonko, kutangaza kuwa hataiunga mkono serikali hiyo.
Tangazo la serikali mpya limekuja takribani wiki mbili baada ya Faye kumfuta kazi Sonko na kulivunja baraza lake la mawaziri kutokana na tofauti za kimtazamo kuhusu uendeshaji wa uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Licha ya kuondolewa serikalini, Sonko ambaye ana ushawishi mkubwa kisiasa nchini Senegal, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge kwa kuungwa mkono na wafuasi wake, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya kuendelea kwa mvutano kati yake na Rais Faye.
Sonko ndiye mwanzilishi na kiongozi mkuu wa chama cha Pastef, kilichoanzishwa mwaka 2014 na ambacho Faye ni mwanachama wake. Chama hicho kina nguvu kubwa bungeni baada ya kushinda viti 130 kati ya 165 vya Bunge la Senegal.
Akizungumza wakati wa kutangaza muundo wa serikali mpya, Waziri Mkuu mpya, Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo, alitaja majina ya mawaziri watakaounda baraza jipya la mawaziri. Hata hivyo, Sonko amesema wazi kuwa chama chake hakitakuwa sehemu ya serikali hiyo.
Msimamo huo wa Sonko unaongeza sintofahamu kuhusu mustakabali wa ushirikiano kati ya viongozi hao wawili waliowahi kuwa washirika wakuu wa kisiasa, huku wachambuzi wakitahadharisha kuwa mzozo huo unaweza kuathiri uthabiti wa kisiasa nchini Senegal.
